Moscow yasisitiza: Marekani inashiriki moja kwa moja katika vita vya Ukraine
-
Vyacheslav Volodin
Vyacheslav Volodin, mkuu wa Duma ya Russia, ameandika kwenye mtandao wa Telegram kwamba Merekani inashiriki moja kwa moja katika operesheni za kijeshi za Ukraine.
Volodin amesema: "Washington inaratibu operesheni za kijeshi nchini Ukraine, na kwa njia hiyo inahusika moja kwa moja katika hatua za kijeshi dhidi ya Russia."
Ameongeza kuwa Washington na wanachama wengine wa NATO barani Ulaya wanaipatia Kiev silaha nzito ili kukabiliana na mashambulizi ya Russia. Marekani na washirika wake wa NATO awali walidai kuwa hawatashiriki moja kwa moja katika vita hivyo ili wasiwe sehemu ya mzozo huo na kuibua vita vingine vya dunia.
Mjumbe wa Russia katika Umoja wa Mataifa pia alisema Jumamosi iliyopita kwamba NATO inapigana na Russia kwa niaba huko Ukraine na kwamba NATO ni tishio kubwa kwa usalama na amani ya kimataifa.
Maafisa hawa wakuu wa Russia wanaashiria nafasi kubwa na ya kimsingi ya Marekani na NATO katika vita vya Ukraine, kutokana na madhara yake. Kwa hakika, tunaweza kusema kuwa, haingewezekana vita hivyo kuendelea kwa miezi mitatu sasa bila ya msaada mkubwa wa silaha wa Marekani na washirika wake kwa serikaIi ya Kiev. Washington na NATO wanaviona vita vya Ukraine kama fursa ya kipekee ya kuidhoofisha Russia, haswa uwezo wake wa kijeshi. Tangu kuanza kwa mashambulizi ya Russia nchini Ukraine, Marekani na nchi za Ulaya zimekuwa zikituma kiwango kikubwa cha silaha nchini humo kuisaidia serikali ya Kiev. Russia kwa upande wake, imeonya mara kwa mara kwamba hatua hiyo inatishia usalama barani Ulaya. Vilevile kumechapishwa ripoti nyingi kuhusu msaada mkubwa wa kijasusi wa Washington kwa Ukraine. Taarifa hizo za kijasusi zinatumiwa na Kiev katika vita kushambulia vikosi vya Russia na kuharibu vifaa vya kijeshi vya nchi hiyo. Mfano wazi wa suala hili ni msaada muhimu wa kijasusi wa Washington kwa Kiev kuhusu taarifa za eneo ilikokuwa meli kubwa zaidi ya kivita ya Russia, "Moskva" kwenye Bahari Nyeusi, ambazo zilipelekea kulengwa na hatimaye kuzamishwa meli hiyo kwa makombora ya kupigia meli ya jeshi la Ukraine. Mfano mwingine wa misaada kijasusi ya Marekani kwa Ukraine na ripoti za kiintelijensia zilizotolewa na Washington kwa Kiev kuhusu eneo walikokuwa majenerali wa Russia karibu na mji wa Kherson kusini mwa Ukraine, ambao walishambuliwa na kikosi maalumu cha jeshi la Ukraine na kuuliwa. Kwa kutumia msaada huo wa kijasusi wa Marekani, Ukraine iliwaua majenerali 12 wa jeshi la Russia. Gazeti la New York Times liliripoti Jumatano, Mei 4, likiwanukuu maafisa wa ngazi za juu wa Marekani kwamba, nchi hiyo imetoa taarifa kwa Ukraine ambayo ilikuwa na mchango mkubwa katika mauaji ya majenerali wa jeshi la Ukraine. Maelezo kuhusu harakati za wanajeshi wa Rusia, maeneo yao na kadhalika ni sehemu ya misaada ya kijasusi ya Marekani kwa Ukraine. Mwenendo huu huenda ukaviingiza vita vya Ukraine katika awamu mpya na kuvirefusha kwa miezi kadhaa.
Serikali ya Marekani imekadhibisha ripoti ya gazeti la New York Times. Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani, Adrienne Watson ametoa taarifa akijibu ripoti hiyo ya New York Times na kusema, Washington haijabadilishana taarifa za kijasusi na Ukraine juu ya mauaji ya majenerali wa Russia.
Licha ya kukanushwa huku, lakini matamshi yaliyotolewa hivi karibuni ya Rais wa Marekani, Joe Biden, kwa mashirika ya kijasusi ya nchi hiyo kuhusu vita vya Ukraine yanaonyesha ukweli tofauti. Biden alisema katika mazungumzo yake na wakuu wa mashirika ya ujasusi na ulinzi wa Marekani kwamba, ripoti za hivi majuzi kuhusu ushirikiano wa kijasusi wa Marekani na Ukraine zina madhara na zinapaswa kukomeshwa.
Wakati huo huo msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amesema kuhusiana na suala hilo kwamba, jeshi Russia linafahamu vyema kwamba Marekani, Uingereza na NATO kwa ujumla zinatoa taarifa za kijasusi na ripoti nyingine kwa wanajeshi wa Ukraine.
Msaada wa kijasusi wa Marekani na NATO kwa Ukraine katika vita vya nchi hiyo na Russia ni sehemu ya lengo jumla la nchi za Magharibi la kurefusha vita vya Ukraine na katika fremu ya kuishinda nchi hiyo kistratijia.