Benki ya Dunia: Misaada ya UN imeshindwa kupambana na umaskini Afghanistan
Benki ya Dunia imetangaza kuwa, hali ya kibinadamu nchini Afghanistan ni mbaya sana na kwamba misaada ya Umoja wa Mataifa imeshindwa kuzuia ukata na umaskini wa kupindukia nchini humo.
Mwezi Abosti 2021, kundi la Taliban lilitwaa tena madaraka nchini Afghanistan. Marekani ilitumia kisingizio hicho kuzuia mali za wananchi wa Afghanistan ambazo zina thamani ya takriban dola bilioni 10. Matokeo yake ni kuzidi kuteseka kwa umaskini wananchi wa Afghanistan.
Benki Kuu ya Afghanistan chini ya utawala wa Taliban imeshindwa kupata njia za kutumia vyanzo na rasilimali za nchi hiyo kimataifa. Kama miaka iliyopita, hadi hivi sasa Afghanistan inahitajia mno kuingiza vitu muhimu na vya dharura kutoka nje kama chakula, madawa na bidhaa nyingine za kimsingi. Kukwamishwa kufanya hivyo ni moja ya sababu za kuongezeka mgogoro wa njaa na umaskini huko Afghanistan.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Benki ya Dunia imesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kabisa kwamba, hali ya kiuchumi na kijamii ya Afghanistan ni mbaya sana na licha ya Umoja wa Mataifa kutoa misaada ya kibinadamu, lakini imeshindwa kuzuia umaskini wa kupindukia nchini humo. Moja ya sababu hizo ni vikwazo ilivyowekewa Afghanistan baada ya kurejea madarakani kundi la Taliban, mwezi Agosti 2021.
Ripoti hiyo imesema, uchumi wa Afghanistan umesambaratika. Hakuna uzalishaji ajira. Vyakula, nishati na bidhaa zote muhimu zinatoka nje, suala ambalo linasababisha mfumuko wa bei na kupanda maisha na hatimaye kuishia kwenye kuongezeka vibaya umaskini nchini humo.