Jun 05, 2016 14:26 UTC
  • Ban Ki moon aomboleza kifo cha Muhammad Ali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mkono wa pole kufuatia kifo cha bingwa na nguli wa ndondi duniani, Muhammad Ali.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa hapa mjini Tehran imenukuu taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa umoja huo akielezea kusikitishwa sana na kifo cha bingwa huyo wa masumbwi duniani na kusema kuwa, Muhammad Ali alikuwa bingwa wa dunia aliyepigania usawa na amani kwa watu wote ulimwenguni.

Ban Ki moon ameongeza kuwa, Muhammad Ali alipigania dunia iliyo bora na alitumia nafasi yake kwa ajili ya kustawisha ubinadamu duniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amegusia pia kazi mbalimbali za kupigania amani na haki za binadamu zilizofanywa na Muhammad Ali na kubainisha kuwa, mwaka 1998, bingwa huyo wa mabingwa katika ndondi aliteuliwa kuwa balozi wa amani wa Umoja wa Mataifa na alifanya kazi kubwa ya kuwasaidia watoto na watu wanaoteseka katika vita na machafuko duniani.

Muhammad Ali alifariki dunia siku ya Ijumaa ya tarehe 3 Juni akiwa na umri wa miaka 74, baada ya kuugua ugonjwa wa kutetemeka kwa muda mrefu.

Tags