Kuuawa kigaidi Shinzo Abe; mwisho wa 'Tina' wa Japan
(last modified Sat, 09 Jul 2022 11:10:32 GMT )
Jul 09, 2022 11:10 UTC
  • Shinzo Abe
    Shinzo Abe

Shinzo Aben, Waziri Mkuu wa zamani wa Japan alifariki dunia Ijumaa asubuhi baada ya kupigwa risasi mbili katika tukio la ugaidi.

Shinzo Abe alipigwa risasi hizo alipokuwa akihutubu katika kampeni za uchaguzi. Dakika chache baada ta tukio hilo, polisi ilimtia nguvuni Tetsuya Yamagami mwenye umri wa miaka 41 na ambaye ni mwanachama wa zamani wa jeshi la wanamaji la Japan kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.

Kuuawa kwa Shinzo Abe ikiwa zimesalia siku mbili pekee kabla ya kufanyika uchaguzi wa bunge ambao umepangwa kufanyika Jumapili tarehe 10 Julai huenda kukaibua wingu maalumu la huruma katika uchaguzi huo.

Na hasa ikitiliwa maanani kuwa kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wa maoni, chama cha Shinzo Abe cha Liberal Democratic, kinatazamiwa kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi huo, jambo ambalo bila shaka litatoa msukomo mkubwa katika juhudi za kuifanyia marekebisho katiba ya Japan.

Shinzo Abe alipoitembelea Iran

Abe ambaye ana rekodi ya kipekee ya kuwa waziri mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Japan, alijiuzulu nafasi hiyo mwaka 2020 kwa sababu za kiafya. Alikuwa Waziri Mkuu wa Japan kwa miaka 8 yaani tokea mwaka 2012 hadi 2020.

Baada ya kuondoka madarakani, Abe alitumia muda wake mwingi kuhudumia kisiasa chama chake cha Liberal Democratic, ambapo katika siku za karibuni alifanya juhudi kubwa za kushiriki katika kampeni za kisiasa katika miji tofauti ya Japan kwa ajili ya kuimarisha nafasi ya chama hicho katika siasa za nchi hiyo.

Mauaji hayo ya kigaidi ambayo yameakisiwa pakubwa katika vyombo vya habari vya dunia yamezingatiwa na kuwahuzunisha wengi katika pembe tofauti za dunia.

Pamoja na ukweli kwamba Japan ina sheria kali kuhusu kubeba silaha na watu wanaweza kutumia tu bunduki za hewa hata wanapopata kibali, Japan ni miongoni mwa nchi chache zilizo na kiwango cha chini zaidi cha mauaji yanayotokana na matumizi mabaya ya silaha moto.

Kwa mfano, mwaka  2014, kuliripotiwa vifo 6 tu vinavyohusiana na matumizi mabaya ya bunduki nchini Japan, ambayo ni tofauti kubwa ikilinganishwa na kesi 33,599 za mauaji nchini Marekani.

Muuaji wa Abe akikamatwa na maafisa usalama

Uchaguzi ujao wa wabunge nchini Japan utafanyika Jumapili huku Shinzo Abe, kiongozi wa chama cha Liberal Democratic, akiwa ameufumbia macho ulimwengu siku mbili tu kabla ya uchaguzi, na huenda tukio hilo la kusikitisha na kutia uchungu likawa sababu ya wanachama wake kupata moyo zaidi wa kufuatilia mipango ya Abe kuhusu siasa zake za ndani na nje ya nchi, ambayo inaweza kuchukuliwa kama urithi wake wa kisiasa na kiuchumi.

Yuki Tatsumi, Mkurugenzi wa Kituo cha Stimson cha Japan huko Washington, anasema kuchaguliwa Yoshihide Suga ashike nafasi ya Abe baada ya kujiuzulu mnamo 2020 ni hakikisho la kuendelea kwa mipango yote ya kisiasa ambayo Shinzo alianzisha.

Abe alikuwa na mipango ya kina ya mageuzi ya kiuchumi nchini Japani, kiasi kwamba mipango hiyo iliitwa "Abenomics" kutokana na taathira zake kubwa nchini humo.

Shinzo Abe

Katika uwanja wa sera za kigeni, Abe alikuwa mtetezi shupavu wa marekebisho ya katiba ya Japan ili iwe na nafasi muhimu katika masuala ya kudhamini usalama wa kimataifa, katiba ambayo iliandikwa kwa kuzingatia hali ya ndani na nje ya Japan baada ya Vita vya vya Pili vya Dunia.

Abe alijaribu kubadilisha kifungu cha 9 cha katiba ya Japan, ambacho kinasema kwamba Japan "inaachana na vita milele kama haki huru ya taifa, na tishio au matumizi ya nguvu kama njia ya kusuluhisha mizozo ya kimataifa," jambo ambalo halijafanikiwa hadi sasa.

Abe, ambaye alihudumu kwa muda mrefu zaidi kama waziri mkuu wa Japan, alikuwa mtu maarufu miongoni mwa watu, hasa wafuasi wa chama cha Liberal Democratic Party, na kwa sababu hiyo akaja kujulikana kwa jina la "Tina" kwa lugha ya Kijapani, ambayo ina maana ya 'chaguo lisilo na mbadala."