Ramadhani, mwezi wa ibada na toba (1)
(last modified Mon, 06 Jun 2016 11:12:31 GMT )
Jun 06, 2016 11:12 UTC
  • Ramadhani, mwezi wa ibada na toba (1)

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika kwenye mwezi mwingine mtukufu wa Ramadhani ili tupate fursa nyingine ya kunufaika na fadhila, baraka na neema zake. Mwezi wa Ramadhani umeingia taratibu ili kutupa fursa nyingine ya kunong'ona na Mwenyezi Mungu na hivyo kutufanya tuwe karibu na neema pamoja na rehema zake zisizo na mwisho.

Mwezi huu umeingia ili kutupa fursa ya kunufaika na siku pamoja na usiku zake katika kuthibitisha ikhlasi na uchaji Mungu wetu kwa Mola wetu Muumba. Kwa hivyo ndugu wasikilizaji, tulio na nyoyo zilizojaa dhambi, njooni tupae mbinguni kwa pamoja kwa kutumia mabawa ya toba ili tupate kunufaika na rehema, msamaha na maghfira ya Mwenyezi Mungu. Salamu ziwe juu yako ewe mwezi uliojaa rehema za Mwenyezi Mungu! Salamu zikufikie ewe mwezi tunaoupenda, uwe karibu nasi daima! Tunakupeni mkono wa heri na fanaka enyi wasikilizaji wapenzi kwa kuwadia mwezi huu mtukufu wa ibada na toba. Katika mwezi huu mtukufu, tutakuwa tukikuleteeni mfululizo wa vipindi maalumu kwa mnasaba huu adhimu, tukitumai kwamba vitatusaidia sote kufuata njia sahihi ya ufanisi na saada ya humu duniani na huko Akhera. Kipindi hiki cha kwanza kitazungumzia masuala tofauti ikiwemo sehemu ya dua ya Makarim al-Akhlaq ya Imam Sajjad (as), visa vya kuvutia vya historia ya Kiislamu na baadhi ya nasaha za Imam Ali kwa mwanawe Imam Hassan (as). Karubuni

********

Dua ya Makarim al-Akhlaq ni miongoni mwa dua za kuvutia za Imam Sajjad mwana wa Imam Hussein (as). Dua hii imejaa madhumuni na misingi muhimu ya kiakhlaqi na kidini. Imam Sajjad ambaye katika kipidi cha baada ya tukio chungu la kuawa kinyama baba yake Imam Hussein (as) huko katika ardhi ya Karbalaa nchini Iraq alikabiliwa na vizingiti vingi pamoja na upotofu mkubwa wa watu wa zama zake, alitumia dua kama njia bora zaidi ya kufundisha na kueneza mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Hata kama dua ambazo zimepokelewa kutoka kwa Imam Sajjad (as) zinabainisha siri na mambo ambayo kwa kawaida mja anapaswa kumuomba Muumba wake wakati wa haja na matatizo, lakini uchunguzi wa kina wa maana ya dua hizo unabaini wazi kwamba, dua hizo zilikuwa na maana kubwa na za kina zaidi kuliko dua za kawaida ambazo mja humuomba Muumba wake anapokabiliwa na upweke, msononeko, migogoro, mashinikizo na matatizo tofauti maishani. Uzingatiaji wa makini wa dua hizo ambazo kidhahiri ni za kuomba msaada wa Mwenyezi Mungu katika utatuzi wa matatizo na kukidhiwa haja, unabaini kwamba dua hizo pia zimebeba ibara na maana kubwa za kisiasa na kijamii. Dua ya Makarim al-Akhlaq imegawanyika katika sehemu 30 muhimum ambapo kila sehemu inaanza kwa kumswalia Mtume (saw) pamoja na Aali zake watoharifu (as) na kisha kuomba mambo ambayo yanaoongoza kwenye akhlaqi na maadili bora. Kwa msingi huo sentensi ya kwanza ambayo Imam Sajjad (as) aliitamka kwenye dua hiyo ni ya kumswalia Mtume (saw) pamoja na Aali zake (as). Sisi pia hapa tunakipamba kipindi chetu hiki kwa kufuata mfano huo wa Imam Sajjad kwa kumswalia Mtume na Aali zake (as): Allahumma Swali Alaa Muhammadin wa Aali Muhammad.

Kumswalia Mtume na Aali zake mwanzoni mwa dua ni kwa ajili ya kujibiwa dua nzima. Hata hivyo ni muhimu kuashiria hapa kwamba huenda dua isijibiwe na Mwenyezi Mungu kutokana na sababu tofauti. Hii ni kwa sababu ni Mwenyezi Mungu, Mjuzi wa mambo yote, ndiye anayejua zaidi maslahi ya mja anayeomba dua kumliko yeye mwenyewe. Kwa mfano ikiwa mtu ataomba dua ya kumtaka Mwenyezi Mungu ambakishe hai daima bila ya kumfisha ni wazi kuwa dua hiyo haitajibiwa kwa sababu Mwenyezi Mungu mwenyewe amesema kuwa kila kilicho hai humu duniani kitaonja mauti na kufa. Ni wazi pia kwamba dua ya mtu anayemuomba Mwenyezi Mungu na kumtaka amfanye aendelee kuwa kijana bila kumzeesha haiwezi kujibiwa. Hii ni kutokana na kuwa tayari Mungu ameshatayarisha na kuainisha hatua tofauti ambazo mwanadamu anapasa kuzipitia kabla hajaaga duani, nazo ni utoto, ujana, utu uzima na kisha kuingia katika kipindi cha uzeeni ambapo taratibu huanza kupoteza nguvu na hata baadhi ya wakati kusahau mambo aliyokuwa akiyajua vizuri.

Mara nyingine watu huomba dua kinyume na kanuni za maumbile au kutokana na ujahili wao kuhusu baadhi ya mambo. Ni kutokana na ukweli huo ndipo baadhi ya wakati Maimamu maasumu walikuwa wakitahadharisha na kuwaonya watu waliokuwa wakiomba dua kama hizo, maonyo ambayo yamerekodiwa katika vitabu vya hadithi. Kwa msingi huo ni wazi kuwa dua zinazokwenda kinyume na kanuni za maumbile ya Mwenyezi Mungu haziwezi kujibiwa. Mbali na hayo dua ambayo daima hujibiwa ni dua ya kumswalia Mtume (saw) na Aali zake watoharifu (as). Kwa msingi huo ili kujibiwa dua zako nyingine, unapasa kwanza kumswalia Mtume na Aali zake kabla ya kuomba dua hizo. Imam Swadiq (as) anasema kuhusiana na suala hilo: "Wakati mmoja wenu anaposimama mbele ya Mwenyezi Mungu kuomba dua, ni sharti aanze dua hiyo kwa kumswalia Mtume. Hii ni kwa sababu kumswalia Mtume hukubaliwa na Mwenyezi Mungu, na Mungu hawezi kujibu sehemu moja (kumswalia Mtume) ya dua iliyo na maombi kadhaa na kutojibu sehemu nyingine ya dua hiyo."

********

Siku moja Mtume (saw) aliwauliza masahaba wake: "Ni nani kati yenu anayefunga daima?" Salman Farisi, mmoja wa masahaba wa karibu wa Mtume alisema: "Mimi ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mtume akauliza tena: "Ni nani kati yenu hukesha kwa ibada kila siku?" Bado Salman alijibu kwa kusema: "Mimi." Mtume aliendelea kuuliza: "Ni nani kati yenu huhitimisha Qur'ani usiku na mchana mara moja?" Mara hii pia Salman alitoa jibu chanya kwa swali hilo la Mtume, jambo lililomkasirisha mmoja wa masahaba wa Mtume aliyekuwa karibu na mahala hapo. Alisema; ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Salman ni Mfarisi na anataka kujifaharisha na kujiona kuwa mbora kutuliko sisi Waarabu wa Kikureishi?! Mimi mara nyingi humuona akila chakula na kulala usiku. Ni vipi huwa anahitimisha Qur'ani kila siku ilhali mimi humuona siku nyingi akiwa amenyamaza tu?!"

Mtume alimwambia: "Ewe Bwana, tulia! Sasa muulize mwenyewe ili akufafanulie anayafanya vipi hayo." Sahaba huyo alimtaka Salman afafanue naye akasema: "Si hivyo unavyodhani wewe! Mimi hufunga siku ya kwanza, ya katikati na ya mwisho ya kila mwezi. Mwenyezi Mungu pia amesema kuwa kila mtu anayefanya jambo jema humpa thawabu za mambo kumi kama hayo. Mimi hufunga hivi kila mwezi na hivyo kupata thawabu za mtu anayefunga kila siku yaani siku zote za mwezi. Ama nimemsikia kipenzi changu, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema: Kila mtu anayelala akiwa msafi, (yaani akiwa na wudhu, ghusl au tayamum), ni kana kwamba amekesha usiku kucha akifanya ibada, na mimi huenda kulala usiku nikiwa msafi. Vilevile nilimsikia Mtume (saw) akimwambia Ali bi Abi Talib (as): Mtu anayesoma mara moja Surat al-Ikhlas kwa siku huwa amesoma thuluthi moja ya Qur'ani, anayesoma mara mbili huwa amesoma thuluthi mbili ya Qura'ni na anayeisoma mara tatu huwa amehitimisha Qur'ani nzima." Kisha Salman akaendelea kusema: "Mimi huisoma sura hii mara tatu kwa siku na kwa hivyo huwa ninaihitimisha Qur'ani kila siku."

********

Nasaha za Imam Ali (as) kwa mwanawe Imam Hassan (as) ni moja ya nasaha mashuhuri zaidi za mtukufu huyo. Alimuusia mwanawe mkubwa nasaha hizo baada ya kutoka katika vita vya Swiffin, nasaha ambazo zimezingatiwa sana na Mashia pamoja na Masuni. Ni wazi kuwa nasaha hizo huo muhimu hazikukusudiwa Imam Hassan pekee bali zinawahusu watu wote wanaotafuta haki na ukweli. Nasaha hizo zimenukuliwa katika barua ya 31 kati ya barua mbalimbali zilizoandikwa na Imam Ali (as) kwa minasaba tofauti. Kabla ya jambo lolote lile Imam anaanza barua hiyo kwa kumuusia mwanawe azingatie taqwa katika kila jambo analolifanya kwa kumwambia: "Wasia na nasaha zangu kwako ni kumwogopa Mwenyezi Mungu na kushikamana na maamrisho yake, kutakasa nafsi yako kwa kumtegemea na kushikamana na kamba yake...."

Nasaha muhimu zaidi aliyompa Imam Ali mwanawe Hassan (as) hapa ni takua ya Mwenyezi Mungu. Umuhimu na nafasi ya takua kwa mwanadamu hasa katika kipindi cha ujana wake huhisika pale matamanio na masuala mengine muhimu ya kipindi hicho yanapotiliwa maanani. Katika kipindi hicho taqwa huwa mfano wa uzio na ngome madhubuti ambayo humkinga na hujuma ya adui, na mfano wa ngao inayomkinga na mishale yenye sumu ya shetani. Kama mnavyojua wapenzi wasikilizaji, mwanadamu daima huwa amesimama kati ya njia panda mbili zilizo na matokeo tofauti yanayogongana maishani. Njia moja humuita kwenye mambo mema na ya heri na ya pili humshawishi kutii matamanio yake ya kishetani yanayokinzana moja kwa moja na maamrisho pamoja na makatazo ya Muumba wake. Katika hali hiyo ni wazi kuwa mtu anayeweza kufanikiwa na kushinda vita hivyo hatari vya wema na uovu, akili na matamanio, heri na ufisadi na utakasifu na uchafu ni yule tu atakayekuwa amejizatiti kwa silaha ya imani na takua na ambaye alianza jihadi ya kupambana na matamanio yake tokea kipindi cha ujana wake. Nabii Yusuf (as) aliweza kushinda mtihani mkubwa na mgumu wa Mwenyezi Mungu na kufikia kilele cha izza na utukufu kwa kutegemea irada na taqwa madhubuti aliyokuwa nayo. Kumwogopa Mwenyezi Mungu na kutii amri zake kama alivyomuusia Imam Ali mwanawe Imam Hassan (as) ni funguo mbili muhimu ambazo humfungulia mwanadamu kufuli za hazina za saada ya humu duniani na huko Akhera. Ni matarajio yetu kwamba inshaallah katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani tutapata fursa na taufiki ya kuimarisha taqwa zetu na kuzifanya kuwa kipimo cha maamuzi na matendo yetu, inshaallah. Huku tukikuageni kutoka hapa studio, tunakuombeni msitusahau kwenye dua zenu, kwaherini.

Tags