Joto kali laua watu zaidi ya 2000 Uhispania na Ureno
Watu zaidi ya 2000 wamepoteza maisha huko Ushipania na Ureno katika wiki za karibuni kufuatia joto kali lililovunja rekodi likiambatana na moto mkubwa wa misituni ambao umelazimisha maelfu ya watu kuzihama nyumba zao.
Watalamu wa mabadiliko ya tabianchi wanasema, wimbi la ongezeko la joto linaloendelea ambalo limezikumba Uingereza, Ufaransa, Uhispania na Ureno katika wiki za karibuni, linaweza kuendelea kwa wiki kadhaa zijazo.
Zaidi ya hekari 1.3 za ardhi ya misitu huko Uhispania, Ufaransa na Ureno zimeungua kwa moto huku wataalamu wakitahadharisha kuwa hali mbaya zaidi bado inakuja."

Huko Uingereza na Ufaransa tahadhari nyekundu imetangazwa kufuatia kuongezeka wimbi la joto kali. Hili ni wimbi la pili la joto kuwahi kuliathiri eneo la mashariki mwa Ulaya katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja.
Tangazo la tahadhari nyekundu lina maana ya kuvurugika pakubwa kwa huduma za afya, shule, na hata vinu vya nyuklia.
Taasisi ya Afya ya Carlos III ya Uhispania imeeleza kuwa, watu 1,047 wamefariki dunia nchini humo kutokana na kuongezeka hali ya joto kati ya Julai 10 hadi 19 mwezi huu.
Nchini Ureno Mkurugenzi Mkuu wa Afya amenukuliwa akisema kuwa, vifo 1,063 vilivyosababishwa na ongezeko la joto nchini humo vilitokea baina ya tarehe 7 na 18 mwezi huu wa Julai.
Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, amesema hali hivi sasa ni ya hatari na kuongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi ni ukweli ambao hauwezi kupingika, huku akiwahimiza wananchi kuchukua tahadhari.
Sanchez amesema takwimu hizo za waliopoteza maisha zimewasilishwa na Taasisi ya Afya ya Carlos III ambayo inakadiria kwamba idadi ya vifo vinavyotokana na joto itaongezeka mwaka huu ikilinganishwa na miaka iliyopita. Kiwango cha joto katika baadhi ya maeneo ya Uhispania kimefikia zaidi ya nyuzijoto 45, na joto hilo limepelekea misitu kuteketea moto.