IMF: Dunia itaendelea kushuhudia kudorora zaidi kwa uchumi
(last modified 2022-07-27T08:03:18+00:00 )
Jul 27, 2022 08:03 UTC
  • IMF: Dunia itaendelea kushuhudia kudorora zaidi kwa uchumi

Ripoti ya hali ya uchumi kwa robo mwaka iliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF imesema, hivi karibuni ulimwengu utashuhudia kudorora kwa uchumi kimataifa na kwamba njia kuu ya kusaidia nchi zote kwa sasa ni kuungana na kushirikiana; na iwapo hazitafanya hivyo kutakuwa na utofauti mkubwa wa ukuaji wa uchumi kijiografia katika siku zijazo.

Hayo yameelezwa na Pierre-Olivier Gourincha, Mkurugenzi wa Idara ya utafiti wa IMF alipozungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya IMF jijini Washington DC nchini Marekani ambapo ameeleza hali ya kiuchumi inazidi kuwa mbaya. 

Gourincha amesema mtazamo umekuwa giza sana tangu mwezi Aprili na akafafanua kwamba, ulimwengu hivi karibuni unaweza kushuhudia kudorora kunakopeleka uchumi wa kimataifa ukingoni, ikiwa ni miaka miwili tu baada ya kushuhudia mdodoro wa mwisho.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya utafiti wa IMF sababu kuu za kudorora kwa uchumi ni kupanda kwa mfumuko wa bei, kupanda kwa viwango vya riba, thamani ya juu ya dola ya kimarekani, athari za vita vya Ukraine na kushuka kwa ukuaji wa uchumi wa China.

Gourincha amesisitiza kuwa, kinachohitajika sasa ni ushirikiano wa pande nyingi katika maeneo mengi ili kupunguza hatari ya dunia kugawanyika; sambamba na kuimarisha ushirikiano, kwa kuwa hiyo ndio njia bora ya kuboresha matarajio ya kiuchumi kwa wote na kupunguza hatari ya kugawanyika kijiografia.

IMF imesema mfumuko wa bei unaoendelea nchini Marekani na mataifa mengine makubwa ya kiuchumi unasababisha Benki Kuu kuongeza viwango vya riba.

Imeelezwa pia kwamba kishawishi kwa sasa kitakuwa nchi kusukuma mageuzi ya kiuchumi au kuongeza matumizi, lakini IMF imeonya kuwa hatua hiyo itakuja kuongeza maumivu zaidi baadaye.../

Tags