Uhispania, Brazil zaripoti vifo vya kwanza vya Monkeypox nje ya Afrika
Vifo vya kwanza vilivyotokana na ugonjwa wa Ndui ya Nyani (Monkeypox) nje ya bara la Afrika vimeripotiwa katika nchi za Uhispania na Brazil, huku maambukizi ya ugonjwa huo yakiongezeka kote duniani hususan barani Ulaya.
Kituo cha Dharura cha Wizara ya Afya ya Uhispania kimetangaza kuwa, mtu mmoja ameaga dunia kwa maradhi hayo katika mripuko wa sasa ulioanza Mei.
Nchi hiyo ya Ulaya inaongoza kwa kuwa na kesi nyingi zaidi za ugonjwa huo duniani, ambapo mpaka sasa imesajili visa visivyopungua 4,298.
Wakati huohuo, Waziri wa Afya wa Brazil, Fabio Baccheretti amesema mtu mmoja aliyekuwa na umri wa miaka 41 ameaga dunia kwa Homa ya Nyani akitibiwa hospitalini katika mji wa Belo Horizonte, kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa WHO, zaidi ya kesi 20,000 za ugonjwa huo zimeripotiwa katika nchi 78 duniani katika mripuko huu mpya, nyingi zikiwa barani Ulaya.

Kituo cha Kuzuia na Kupambana na Magonjwa Afrika (Africa CDC) kimesema kufikia sasa kesi 2,101 za maradhi hayo zimeripotiwa barani Afrika, mbali na vifo 75 tangu mwanzoni mwaka huu 2022.
Hata hivyo taasisi hiyo ya Umoja wa Afrika imesema kesi zilizothibitishwa hadi sasa barani humo ni 283, huku kesi 1,818 zikishukiwa kuwa za ugonjwa huo.
Siku chache zilizopita Shirika la Afya Duniani (WHO) liliutangaza ugonjwa wa Ndui ya Nyani (Monkeypox) kuwa tishio la afya duniani.