Jun 02, 2026 03:11 UTC
  • Leo katika Historia
    Leo katika Historia

Leo ni Jumanne tarehe 16 Dhulhija 1447 Hijria sawa na tarehe Pili Juni 2026.

Miaka 976 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Abu Abdullah Muhammad bin Jiyani, mnajimu na mwanahisabati wa Kiislamu huko Andalusia.

Alizaliwa mwaka 379 Hijiria huko Cordoba moja ya miji ya kale ya Uhispania na alisoma hadi kuhitimu katika mji huo huo. Baada ya hapo alikwenda katika mji mkuu wa Misri, Cairo na kuishi huko kwa miaka minne.

Jiyani alikuwa mahiri mkubwa katika elimu ya nujumu na miongoni mwa athari za mwanahisabati huyo ni kitabu chake cha nujumu ambacho kimetajwa katika makala ya 5 ya kitabu cha elementi cha baba wa jiometri, Euclid wa Ugiriki ya kale.  ****

Katika siku kama hii ya leo miaka 144 iliyopita alifariki dunia Giuseppe Garibaldi kamanda mzalendo na kiongozi wa harakati ya kuimarisha umoja wa Italia.

Giuseppe alizaliwa mwaka 180 na wakati wa ujana wake alifanya kazi mbalimbali na mwishowe alijiunga na jeshi. Baadaye alichaguliwa kuwa kamanda wa wanaharakati wa kupigania uhuru wa Italia na alifanya jitihada kubwa za kujenga umoja nchini humo. Kwa sababu hiyo alijulikana katika historia ya Italia kama shujaa wa taifa. ***

Siku kama ya leo Miaka 56 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf nchini Iraq aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92.

Baada ya kuaga dunia Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa mar'ja' mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, Ayatulah Hakim alichukua nafasi yake na kufuatwa na Waislamu wengi na hasa wa Iraq, kuhusiana na masuala ya kifik'hi. Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu. Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq.

Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel. Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu.  ***

Miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo,  sawa na tarehe 12 Khordad mwaka 1379 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Hujjatul Islam Sayyid Ali Akbar Abuturabi, mwanzuoni mwenye mwamko na mwanaharakati wa Iran katika ajali ya gari pamoja na baba yake Ayatullah Sayyid Abbas Abuturabi.

Hujjatul Islam Sayyid Ali Akbar Abuturabi alizaliwa mwaka 1318, kwa mujibu wa kalenda ya Iran, katika mji wa kidini wa Qum. Alijifunza elimu ya dini kutoka kwa maulamama wakubwa akiwemo Imam Khomeini (M.A). Hujjatul Islam Abuturabi katika mapambano ya kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu mara kadhaa alikamatwa na kuteswa na vibaraka wa Shah.

Wakati vya vita vya Iran na Iraq mwaka 1359 Hijria Shamsia alikamatwa mateka na askari wa utawala wa Baath wa Iraq na kufungwa kwa miaka 10 katika jela zenye mateso makali za Iraq. Lakini alivumilia kiasi cha kuwa mashuhuri miongoni mwa mateka wa Iran kwenye jela hizo. Alipoachiliwa huru aliteuliwa kuwa mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya mateka na walioachiliwa huru.  ***

Tarehe Pili Juni ni Siku ya Taifa ya Uingereza.

Nchi ya kisiwa ya Uingereza yenye eneo lenye ukubwa wa zaidi ya kilomitamraba 244,000 inapatikana upande wa Magharibi ya Ulaya na baina ya bahari za Atlantiki, Manche, bahari ya kaskazini na Bahari ya Ireland. Uingereza ina idadi ya watu wanaokaribia milioni 60. Mfumo wa utawala wa nchi hiyo ni wa kifalme, lakini mamlaka ya utendaji ya serikali yako mikononi mwa waziri mkuu.

Akthari ya Waingereza ni wafuasi wa madhehebu ya Anglikana ambalo ni tawi la madhehebu ya Kikristo ya Protestanti. Uingereza imetokana na muungano wa Scotland, England, Wales na Ireland ya Kaskazini. Maeneo hayo kila moja lina mamlaka maalumu ya kujiendeshea mambo yake ya ndani. Tarehe Pili Juni, ambayo ni siku aliyozaliwa Malkia, inajulikana kuwa Siku ya Taifa ya Uingereza. ***