Guterres: Wanaadamu wanacheza na bunduki iliyosheheni risasi
-
Antonio Guterres
Katika kumbukumbu ya miaka 77 ya shambulio la mabomu ya nyuklia ya Marekani dhidi ya Japan, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba ubinadamu unacheza na bunduki iliyosheheni risasi katika anga ya migogoro ya sasa ya hatari ya nyuklia.
Antonio Guterres alikuwa akihutubia Mkutano wa 10 wa Mapitio ya Mkataba wa Kuzuia Silaha za Nyuklia (NPT) ambao hatimaye ulianza Jumatatu iliyopita kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York baada ya kuahirishwa mara kadhaa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitahadharisha nchi wanachama wa NPT kwamba ulimwengu unakabiliwa na hatari ya vita vya nyuklia ambayo haijawahi kuonekana tangu wakati wa Vita Baridi, na kwamba kosa moja la kimahesabu linaweza kusababisha maangamizi ya nyuklia.
Mkataba wa Kuzuia Ueneza Silaha za Nyuklia (NPT), ambao ulianza kutumika mwaka 1970, umetiwa saini na zaidi ya nchi 191 duniani.
Antonio Guterres, aliyekuwa akihutubia shughuli ya kila mwaka ya kukumbuka mashambulizi ya nyuklia ya Marekani dhidi ya Japan iliyofanyika Hiroshima kuwaenzi wahanga wa shambulio la bomu la nyuklia la mwaka 1945, amewaomba kwa dhati viongozi wa dunia kuondoa silaha za nyuklia kwenye maghala yao.
Amesema: "Miaka 77 iliyopita makumi ya maelfu ya watu waliuawa ghafla katika mji huu, na wanawake, watoto na wanaume waliteketezwa kwa moto wa Jahannam; manusura pia wameathiriwa na mionzi ya saratani na magonjwa mengine."

Katibu Mkuu wa UN amesisitiza kuwa migogoro ya kinyuklia inapanuka zaidi na mwanadamu unacheza na bunduki iliyoshehenii risasi.
Watu laki moja na elfu 40 waliuawa katika shambulizi la bomu la atomiki la Marekani huko Hiroshima mnamo Agosti 6, 1945.
Siku tatu baadaye, Marekani ilirusha bomu jingine la nyuklia kwenye mji wa bandari wa Nagasaki na kuua watu wengine 74,000.