Aug 29, 2022 02:33 UTC
  • Undumakuwili wa Marekani kuhusu suala la uhuru wa kujieleza

Kufuatia matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Nader Hashemi, Mhadhiri na Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Denver, kuhusiana na uwezekano wa Israel kuhusika katika shambulio dhidi ya Salman Rushdie, Warepublican katika Congress ya Marekani wameonya kuhusu ushawishi wa Iran katika vyuo vikuu vya nchi hiyo na kutangaza kwamba watachunguza suala hilo katika miezi ijayo.

Katika mahojiano ya hivi karibuni, Nader Hashemi alisema kwamba kutokana na upinzani wa Israel dhidi ya kufufuliwa mapatano ya JCPOA, huenda shirika la ujasusi la utawala huo Mossad, lilimchochea mvamizi wa Salman Rushdie kumdunga kisu ili kuvuruga mapatano hayo.

Maafisa wanaosimamia siasa za kigeni wa Chama cha Republican wametahadharisha kuwa, matamshi hayo yanaonyesha kupanuka kwa ushawishi wa kipropaganda wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika taasisi za kielimu za Marekani. Greg Steube, mjumbe wa chama cha Republican katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, amesema: "Kauli ya mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Denver kuhusu nafasi ya Israel katika shambulio dhidi ya Salman Rushdie ni hatari na si ya kweli na itasababisha kuongezeka chuki dhidi ya Mayahudi katika vyuo vikuu vya Marekani."

Maafisa hao wamesisitiza kuwa katika miezi ijayo wataanza kuzichunguza taasisi kama vile Chuo Kikuu cha Denver ili kukabiliana na kile walichokitaja kuwa chuki dhidi ya Mayahudi na kuenea kwa nadharia za kipropaganda dhidi ya Marekani.

Image Caption

 

"Jim Banks" (3), mjumbe wa chama cha Republican katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, amesema: Nadharia za njama za chuki dhidi ya Mayahudi na Marekani sasa zinaenea katika vyuo vikuu vya Marekani na kutia sumu akilini mwa wanafunzi. "Warepublican wanapaswa kufuatilia wahadhiri wanaoeneza propaganda za chuki za serikali ya Iran dhidi ya Mayahudi."

Warepublican wanasema kuwa wanaandaa miswada kadhaa ya kukabiliana na kile kinachodaiwa ni ushawishi wa nchi za nje, haswa Iran na Uchina, katika taasisi za kielimu za Marekani ili kuiwasilisha kwenye bunge lijalo, ambapo kuna uwezekano mkubwa kwamba Warepublican watakuwa na wingi wa viti.

Msimamo mkali wa viongozi wa chama cha Republican dhidi ya Nader Hashemi mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Denver kwa mara nyingine umeangazia undumakuwili wa wazi uliopo katika suala zima la uhuru wa kujieleza nchini Marekani.

Wakati mhadhiri huyu wa chuo kikuu ameeleza tu mtazamo wake kuhusu shambulio lililofanyika dhidi ya Salman Rushdie, amekuwa akilengwa kwa maneno makali ya chuki na bila shaka ataanza kufuatiliwa na maafisa wa usalama wa Marekani kwa kuzingatia mashinikizo makubwa yanayotolewa dhidi yake na wanachama wa Republican.

Lakini swali ni je, ni sheria gani ya Marekani aliyoivunja kwa kutoa maoni yake, au maoni hayo kuhusu uwezekano wa utawala wa Kizayuni kuhusika katika shambulio dhidi ya Salman Rushdie yana uhusiano gani na suala la chuki dhidi ya Mayahudi? Je, maoni yoyote kuhusu Israeli ni sawa na kuchukua msimamo dhidi ya Mayahudi?

Ikiwa hali ni hivyo basi taarifa na ripoti za mashirika ya kutetea haki za binadamu na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa zinazokosoa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina zinapaswa kuchukuliwa kuwa ni chuki dhidi ya Uyahudi. Ni wazi kuwa Umoja wa Mataifa na nchi nyingi za dunia hazina mtazamo huo bali zinaamini kuwepo tofauti kati ya utawala wa Kizayuni na Mayahudi. Ni kwa msingi huo ndipo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikawa inasisitiza mara kwa mara juu ya kuwepo tofauti kati ya Uzayuni na Uyahudi.

Undumakuwili wa nchi za Magharibi kuhusu suala la uhuru wa kujieleza

Nukta nyingine inayopaswa kuzingatiwa katika muktadha huu ni kwamba Wamagharibi, wakiwemo Wamarekani, wanahalalisha vitendo kama vile vya kuchapishwa vibonzo na vikatuni vya kumdhalilisha Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw) na vile vile kuchapishwa kitabu cha kufuru cha "Aya za Shetani" kwa kisingizio cha kutetea uhuru wa kujieleza. Tathmini ya undumakuwili wa nchi za Magharibi ikiwemo Marekani kuhusu uhuru wa kujieleza, inaonyesha wazi kuwa suala hilo huzingatiwa na nchi hizo pale tu linapohusiana na kudhalilishwa na kukosewa heshima matukufu ya Kiislamu. La sivyo, kutiliwa shaka masuala kama vile mauaji ya lolocaust na kuzungumziwa uwezekano wa utawala wa Kizayuni kuhusika katika shambulio dhidi ya Salman Rushdie huwa hakuruhusiwi kabisa na wanaopatikana na hatia katika uwanja huo hukabiliwa na radiamali kali ya nchi hizo zinazodai kutetea haki za binadamu na uhuru wa kujieleza duniani.

Tags