Mtetemeko wa ardhi waua watu 66 nchini China
Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mtetemeko mkubwa wa ardhi uliotokea nchini China imefikia watu 66 huku mamia ya wengine wakijeruhiwa.
Mtetemeko huo mkubwa wa ardhi wenye ukubwa wa 6.8 kwa kipimo cha rishta ulitokea Jumatatu katika kaunti ya Luding, katika mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa nchi.
Maafisa wa serikali katika mkoa huo wamesema mbali na watu 250 kujeruhiwa kwenye janga hilo la kimaumbile, wengine 16 wametoweka.
Mtetemeko huo umesikika pia katika mikoa ya Shaanxi na Guizhou, mamia ya kilomita kutoka mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa nchi, ambapo zilzala yenye ilitokea.
Zilzala hiyo imekata mawasiliano ya simu na kusababisha maporoko ya udongo na uharibifu wa mali za umma. Habari zinasema kuwa, yumkini idadi hiyo ikaongezeka, kutokana na kukwama watu kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka kutokana na mtetemeko huo.
Miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mtetemeko huo ni Chengdu, makao makuu ya mkoa wa Sichuan, ambao wakazi wake milioni 21 mpaka sasa wapo chini ya sheria kali za kupambana na ugonjwa wa Covid-19.