Kwa nini Biden amekataa kuitangaza Russia kuwa ni nchi inayofadhili ugaidi?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i87952-kwa_nini_biden_amekataa_kuitangaza_russia_kuwa_ni_nchi_inayofadhili_ugaidi
Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Marekani, White House, Karine Jean-Pierre alitangaza Jumanne wiki hii kwamba uamuzi wa Joe Biden wa kutoitangaza Russia kuwa ni mfadhili ugaidi ni wa mwisho.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 09, 2022 02:45 UTC
  • Kwa nini Biden amekataa kuitangaza Russia kuwa ni nchi inayofadhili ugaidi?

Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Marekani, White House, Karine Jean-Pierre alitangaza Jumanne wiki hii kwamba uamuzi wa Joe Biden wa kutoitangaza Russia kuwa ni mfadhili ugaidi ni wa mwisho.

Rais wa Marekani, Joe Biden, alisema siku ya Jumatatu iliyopita kwamba Russia haipaswi kuarifishwa kama nchi inayofadhili ugaidi.

Akizungumzia usafirishaji wa chakula na safari za meli kupitia Bahari Nyeusi, msemaji wa Ikulu ya White House alisema kuwa kutangazwa Russia kuwa ni nchi inayounga mkono ugaidi kunaweza kuwa na taathira mbaya kwa usafirishaji wa chakula.

Msimamo wa Biden wa kutoitambua Russia kama nchi inayofadhili ugaidi unakinzana na msimamo wa Bunge la Marekani (Congress) katika suala hili. Tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine, Congress limechukua mkondo wa kukabiliana na Russia, na katika kesi mbalimbali limetaka kuzidishwe mashinikizo dhidi ya Moscow, ikiwa ni pamoja na kuiwekea vikwazo vya kila aina, na pia kutoa ombi zito la kuitangaza Russia kuwa ni taifa linalofadhili ugaidi. Mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu wa 2022, Seneti ya Marekani ilipitisha kwa kauli moja azimio linalomtaka Waziri wa Mambo ya Nje, Anthony Blinken, kuitangaza Russia kama mfadhili wa ugaidi eti kwa vitendo vyake huko Chechnya, Georgia, Syria na Ukraine. Azimio hilo lisilo na nguvu ya kuilazimisha chochote Serikali, lilitolewa na Seneti kwa lengo la kuweka shinikizo zaidi kwa utawala wa Biden kukabiliana na Moscow. Hapo awali, Joe Wilson, mwakilishi wa Republican huko South Carolina, na Ted Liu, mwakilishi wa Kidemokrati wa California, waliwasilisha muswada sawa na huo katika Baraza la Wawakilishi na kutaka serikali ya Russia itambuliwe kama mfadhili wa ugaidi. Kwa mujibu wa sheria za Marekani, Wizara ya Mambo ya Nje ndiyo yenye jukumu la kutangaza na kuitambulisha nchi yoyote kama mfadhili wa ugaidi. Hitilafu za maafisa wa Marekani juu ya suala la kuitambua Russia kuwa ni dola linalofadhili ugaidi zingali zinaendelea licha ya kuidhinishwa kwa azimio la Seneti linaloitaja Russia kuwa "mfadhili wa ugaidi", na mashinikizo yanayofanywa kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani yakiitaka ihalalishe na kupasisha azimio hilo.

Congress ya Marekani

Russia kwa upande wake imeonya kuwa jambo kama hilo litakuwa na maana ya kuvunjika kabisa uhusiano kati ya Washington na Moscow. Hatupaswi pia kusahau kwamba, hatua hiyo ya Bunge la Marekani inaendana na ombi la Volodymyr Zelenskyy, Rais wa Ukraine, ambaye mara kwa mara amekuwa akitaka Russia itangazwe kama mfadhili wa ugaidi. Hapana shaka yoyote kwamba, kutimia kwa jambo hili, yaani kutangazwa Russia kuwa nchi inayofadhili ugaidi, kutakuwa na matokeo kadhaa mabaya ya kisiasa. Mojawapo ni kusitishwa ushirikiano wa aina yoyote au msaada baina ya Marekani na Russia. Serikali ya Biden pia haitaweza kufanya makubaliano ya aina yoyote au kuomba usaidizi katika nyanja zinazohusiana na shughuli za kibiashara na kiuchumi kwa Russia, kama vile suala la kuagiza bidhaa za kimkakati za chakula au mbolea ya kemikali ya nchi hiyo.

Sababu nyingine ya upinzani wa serikali ya Biden dhidi ya mashinikizo ya kuitangaza Russia kuwa ni nchi mfadhili wa ugaidi ni kwamba hatua kama hiyo itafanya mazungumzo ya baadaye baina ya Washington na Moscow kuwa magumu na tata zaidi.

Jambo muhimu ni kwamba mzozo kati ya Ikulu ya White House na Bunge la Congress kuhusu suala la kuitambua Russia kama mfadhili wa ugaidi unaonesha kuongezeka kwa mpasuko na ufa kati ya mihimuli hiyo miwili ya utendaji na kutunga sheria ya Merekani, na kwa njia fulani, ni ishara ya  ukosefu wa mshikamano wa ndani katika uwanja wa sera za kigeni. Mfano wa wazi wa ukweli huu ni upinzani wa Joe Biden dhidi ya ziara ya Spika wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi, huko Taiwan. Pelosi alipuuza athari na matokeo hatari ya hatua hiyo, na hatimaye akafanya safara huko Taiwan; jambo ambalo liliikasirisha sana China iliyochukua hatua kadhaa za kuiadhibu Marekani. Safari hiyo ya Pelosi pia ilishadidisha hatua za kijeshi za China dhidi ya Taiwan ambazo zinaendelea hadi sasa na kusababisha matatizo mengi kwa serikali ya Taipei.