Kikao cha CICA chamalizika kwa kutiwa saini hati sita za ushirikiano
Wakuu wa nchi wanachama wa Kongamano Kuhusu Maingiliano na Hatua za Kujenga Hali ya Kuaminiana Barani Asia (CICA) wamemalizika mkutano wao huko Astana katika mji mkuu wa Kazakhstan kwa kuidhinisha hati 6 za ushirikiano.
Baada ya kumalizika kikao hicho, Ikulu ya Kremlin ya Russia imetoa taarifa na kuthibitisha kuwa hati sita za ushirikiano zimetiwa saini.
Taarifa ya Astana, ambayo inachukuliwa kuwa hati muhimu zaidi ya ushirikiano kati ya wakuu wa nchi wanachama kwa hatua za maingiliano na hatua za kujenga hali ya kuaminiana huko Asia (CICA), ilitiwa saini na wakuu wa shirika hilo mwishoni mwa mkutano wa Astana. Kulingana na taarifa hiyo, CICA inatazamiwa kubadilika kutoka muundo wa sasa wa 'Kongamano' na kuwa 'Shirika. Mabadiliko hayo yatawezesha CICA kujihusisha na masuala muhimu zaidi na yenye ushawishi kimataifa.
Katika Azimio la Astana, kuna ushirikiano wa kuhakikisha usalama wa teknolojia ya habari na mpango wa utekelezaji wa Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Ugaidi.
Uamuzi wa mkutano wa kilele wa CICA wa kutoa uanachama kwa Kuwait, uamuzi wa uwenyekiti wa mkutano huo mwaka wa 2024 pamoja na kufanya mikutano ya mara kwa mara ya Baraza la Viongozi na Baraza la Mawaziri pia uliidhinishwa na wanachama wakati wa mkutano wa Astana. Aidha sheria ya Mfuko wa CICA pia imeidhinishwa.
Bila shaka, kuundwa kwa utaratibu wa dunia yenye pande kadhaa zenye kuchukua maamuzi yaani multilateralism kwa lengo la kupambana na madola ya kibeberu kama vile Marekani ni mojawapo ya malengo yaliyofafanuliwa ya jumuiya na mashirika ya Asia.
Ni dhahiri kwamba uwepo na ushiriki wa Iran, Russia, China na India katika CICA una maana maalum. Maana hii maalum inahusishwa na mwisho wa mfumo wa kibeberu wa maamuzi ya upande mmoja yaani unilateralism ambao kinara wake ni Marekani..
Kwa msingi huo, vyombo vya habari vyenye mfungamano na Marekani na harakati ya kimataifa ya Kizayuni daima vinaeleza wasiwasi kuhusu kuibuka mrengo wenye kukabiliana na sera za upande mmoja za Marekani. Kwa mfano, hapo awali, wachambuzi wa tovuti ya Kizayuni ya "J Post" waliandika hivi katika ripoti kuhusu mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na Kongamano Kuhusu Maingiliano na Hatua za Kujenga Hali ya Kuaminiana Barani Asia (CICA) nchini Kyrgyzstan na Tajikistan:
"Ikiwa unataka kuona jinsi ulimwengu utakavyokuwa bila ushawishi wa Marekani, unaweza kuhudhuria mkutano wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai nchini Kyrgyzstan kama mwangalizi, na kisha kushiriki katika Mkutano wa Kongamano Kuhusu Maingiliano na Hatua za Kujenga Hali ya Kuaminiana Barani Asia (CICA) huko Tajikistan siku ya Jumamosi."
Wasiwasi huo wa vyombo vya habari vya Kizayuni vya Marekani na kimataifa unaonyesha ukweli kwamba viongozi wa Ikulu ya Marekani tayari wana wasiwasi kuhusu kutengwa nchi hiyo katika karne ya 21. Harakati hatari ya Uzayuni pia iko katika mgogoro kwa sababu inapoteza msaidizi wake mkuu duniani, yaani Marekani.
Hata hivyo, mkutano wa Astana na maazimio ya mkutano huo yamefichua ukweli kwamba nchi muhimu zilizowahi kuchukuliwa kuwa washirika wa Marekani sasa zinashiriki katika kushindana kukabiliana na nchi hiyo ya kibeberu katika maeneo tofauti duniani.
Wakati huo huo, hakuna shaka kwamba nchi wanachama wa CICA, ambazo zinaunda asilimia 90 ya eneo la bara la Asia mbali na kuwa makao ya karibu nusu ya idadi ya watu ulimwenguni, zinashiriki katika asasi hii ya kimataifa. CICA leo ina wanachama 28 ambapo mwanachama mpya ni Kuwait. Wanachama muhimu wa CICA ni pamoja na Iran, Russia, China, India, Uturuki, Qatar, Kazakhstan na Uzbekistan. Kwa kubadilisha hadhi ya asasi hiyo ya kimataifa kutoka "Kongamano" hadi "Shirika", inatarajiwa kwamba CICA, kama Shanghai, itakuwa shirika lenye ushawishi mkubwa katika kiwango cha bara la Asia na ulimwengu katika karne hii.