Russia yaonya baada ya US kupeleka silaha mpya za nyuklia Ulaya
Russia imekosoa vikali hatua ya Marekani ya kupeleka silaha mpya za kisasa za nyuklia za B61 katika kambi za Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) barani Ulaya na kuonya kuwa, ikilazimu, Moscow itatoa jibu kali kwa kitendo hicho.
Shirika la habari la RIA limemnukuu Alexander Grushko, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia akisema kuwa, "Hatuwezi kupuuza mipango ya kuunda upya silaha za nyuklia, na hayo mabomu (ya nyuklia) yaliyoko Ulaya."
Amesema Moscow huenda ikalazimika kutazama upya mikakati yake ya kijeshi, kutokana na hatua ya Marekani ya kuzikarabati na kuziongezea usahihi wa kupiga shabaha silaha hizo za nyuklia zilizorundikana katika nchi za Ulaya.
Mapema mwezi huu, Rais Joe Biden wa Marekani alionya kuhusu hatari ya kutokea 'Kiyama' cha nyuklia wakati huu ambapo Washington imeshadidisha kampeni za kuituhumu Russia kuwa inapanga kutumia silaha za nyuklia nchini Ukraine.
Hii ni licha ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) kutangaza hivi karibuni kuwa hakuna dalili kwamba Rais wa Russia, Vladimir Putin ana mpango wa kutumia silaha za nyuklia.

Tangu vilipoanza vita na mapigano nchini Ukraine mwezi Februari, hatua ya nchi za Magharibi ikiwemo Marekani ya kushadidisha mashinikizo ya vikwazo dhidi ya Russia na kupeleka shehena za silaha nyepesi na nzito nchini Ukraine, si tu haijasaidia kutuliza hali ya mambo, bali imekoleza zaidi moto wa vita ndani ya nchi hiyo ya Ulaya.
Haya yanajiri huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akionya kuhusu hatari ya kutokea vita vya nyuklia duniani. Alitoa onyo hilo Agosti Mosi mwaka huu wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Kuangaliwa Upya Mkataba wa NPT wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia.