Italia yatangaza kusitisha kuipelekea silaha Ukraine
(last modified Thu, 03 Nov 2022 06:57:08 GMT )
Nov 03, 2022 06:57 UTC
  • Italia yatangaza kusitisha kuipelekea silaha Ukraine

Serikali ya Italia imetangaza kuwa imesitisha kuipelekea silaha Ukraine ambazo ilikuwa ikizipeleka huko kwa kisingizio cha kupambana na Russia na kutekeleza maazimio ya Jeshi la Nchi za Magharibi NATO.

Gazeti la Il Mesagro‎ la Italia limetangaza habari hiyo na kudai kuwa, serikali ya Rome ambayo ilikuwa ikiipelekea silaha Ukraine chini ya mwavuli wa NATO, imeamua kusitisha kuipa silaha nchi hiyo. Hata hivyo, taarifa hiyo haikusema sababu ya uamuzi huo wa Italia.

Hii ni katika hali ambayo mara chungu nzima Russia imekuwa ikizilaumu nchi za Magharibi kwa kuipa silaha Ukraine ikisisitiza kuwa, hatua hiyo inapelekea kuzidi kuangamizwa Ukraine na kurefuka vita hivyo, bali jambo hilo lina madhara yasiyotabirika hasa kwa Ukraine na wananchi wake.

Nchi za Magharibi zinairundikia silaha Ukraine. Matokeo yake ni kuteteketezwa kwa vita nchi hiyo

 

 

Pamoja na kuweko hasara kubwa za kisiasa, kijeshi, kijamii, kiuchumi na hata kiutamaduni za vita vya Ukraine, lakini nchi za Magharibi ndio kwanza zinaendelea kupiga ngoma ya vita na hazioneshi nia yoyote ya kukomesha vita hivyo.

Nchi za Magharibi hasa Marekani zinazidisha mashinikizo yao dhidi ya Russia katika kila kona mpaka kwenye masuala ya kiutamaduni na michezo. Zinazidi kuirundikia silaha Ukraine, silaha ambazo hata haziwezi kutumika kupiga ardhi ya Russia. Matokeo yake ni kuwa vita baina ya nchi za Magharibi na Russia vinapiganwa ndani ya ardhi ya Ukraine na ni Ukraine na wananchi wake ndio wahanga wakuu wa vita hivyo.

Hayo yamekuja katika hali ambayo, Rais Vladimiri Putin wa Russia amesisitiza kuwa, Umoja wa Ulaya unajaribu kuifuta Moscow katika masuala ya kimataifa kwa kutumia njama mbalimbali lakini hiyo ni ndoto na ni jambo lisilowezekana kabisa.