Maelfu waandamana Italia kuishinikiza Rome isiunge mkono vita vya Ukraine
Maelfu ya wananchi wa Italia wamefanya maandamano katika mji mkuu Rome, kulalamikia hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kuunga mkono vita vinavyoendelea Ukraine.
Maelfu ya Wataliano walikusayika mjini Rome jana Jumamosi, huku wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe za kulaani uungaji mkono wa serikali yao kwa vita vya Ukraine, baadhi ya jumbe hizo zikisema 'Hapana kwa Vita.'
Serikali mpya inayoongozwa na Waziri Mkuu, Giorgia Meloni mara kadhaa imetangaza utayarifu wake wa kuiunga mkono serikikali ya Kiev katika vita dhidi ya Russia.
Haya yanajiri licha ya serikali hiyo ya Italia kutangaza hivi karibuni kuwa imesitisha kuipelekea silaha Ukraine. Rome imekuwa ikizipeleka silaha hizo huko Ukraine kwa kisingizio cha kupambana na Russia na eti kutekeleza maazimio ya Shirika la Jeshi la Nchi za Magharibi NATO.
Gazeti la Il Mesagro la Italia lilitangaza habari hiyo na kudai kuwa, serikali ya Rome ambayo ilikuwa ikiipelekea silaha Ukraine chini ya mwavuli wa NATO, imeamua kusitisha kuipa silaha nchi hiyo. Hata hivyo, taarifa hiyo haikusema sababu ya uamuzi huo wa Italia.
Wananchi wa Italia kama nchi nyingi za Ulaya, wamekuwa wakifanya maandamano katika siku za hivi karibuni kulalamikia gharama ya juu ya maisha, huku wakishinikiza kutafutia ufumbuzi mgogoro wa nishati.
Usambazaji wa gesi ya Russia kuelekea barani Ulaya umepungua kwa kiasi kubwa sana kutokana na vikwazo vya Magharibi dhidi ya Moscow, baada ya Russia kuanzisha mashambulizi dhidi ya Ukraine.