Dec 20, 2022 03:26 UTC
  • Wabunge wa Marekani wataka Trump ashitakiwe kwa uchochezi

Wabunge wa Marekani wanaochunguza shambulio dhidi ya jengo la Congress lililosababisha mauaji na uharibifu mkubwa wamependekeza rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump afunguliwe mashitaka ya uchochezi.

Katika kikao cha wazi jana Jumatatu, wabunge hao wa Kongresi ya Marekani walipasisha kwa sauti moja kupitia kura, hoja ya kutaka Trump ashitakiwe kwa kuchochea ghasia na uasi.

Wameitaka Wizara ya Sheria ya Marekani imfungulie rais huyo wa zamani wa nchi hiyo mashitaka manne ya jinai, yakiwemo ya kuchochea, kushajiisha na kuunga mkono uasi na uvamizi, kula njama ya kulilaghai taifa, na vilevile kula njama ya kuipa serikali ya federali ya nchi hiyo ushahidi wa urongo.

Ikumbukwe kuwa, arehe 6 Januari mwaka jana 2021 wafuasi wa Donald Trump walilivamia jengo la Congress na kufanya mauaji na uharibifu mkubwa.

Wafuasi hao sugu wa Trump walilivamia jengo hilo baada ya rais huyo wa zamani wa Marekani kutuma ujumbe mbalimbali wa maandishi na video katika mitandao ya kijamii hasa Twitter na kuwachochea wafuasi wake wafanye fujo.

Wafuasi wabaguzi wa Trump waliojizatiti kwa silaha

Watu wasiopungua 6 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati wafuasi wa Trump walipolivamia jengo la Congress Jumatano ya tarehe 6 Januari 2021.

Uvamizi wa wafuasi wake hapo tarehe 6 Januari mwaka jana ulifanyika baada ya mabaraza mawili ya Congress, lile la Wawakilishi na lile la Senate kukutana ili kupasisha ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa Rais wa Novemba 23, 2020 huko Marekani.

Tags