Zelenskyy adai: Kuipatia Ukraine misaada ni kuwekeza katika demokrasia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i91994-zelenskyy_adai_kuipatia_ukraine_misaada_ni_kuwekeza_katika_demokrasia
Rais wa Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine ameiambia Kongresi ya Marekani kwamba, kuipatia nchi yake misaada ni sawa na kuwekeza katika demokrasia na si suala la kujitolea.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 22, 2022 07:35 UTC
  • Zelenskyy adai: Kuipatia Ukraine misaada ni kuwekeza katika demokrasia

Rais wa Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine ameiambia Kongresi ya Marekani kwamba, kuipatia nchi yake misaada ni sawa na kuwekeza katika demokrasia na si suala la kujitolea.

Akizuzungumza ndani ya Kongresi ya Marekani katika ziara yake ya ghafla nchini humo, Rais wa Ukraine amewashukuru viongozi na wananchi wa Marekani kwa kuiunga mkono nchi yake katika kile alichokitaja "mapambano dhidi ya Russia."

Marekani imetangaza kuiongezea Ukraine msaada wa kijeshi wa dola bilioni 1.85 ikiwa ni pamoja na kupelekea Ukraine mfumo wa makombora wa Patriot. Msemaji wa Ikulu ya Rais Russia, Kremlin, Dmitry Peskov naye ameeleza kuwa, hatua ya nchi za Magharibi ya kuzidisha misaada yao ya silaha na zana za kijeshi kwa Ukraine itachochea zaidi mgogoro huo. Matamshi haya ni jibu rasmi kutoka kwa afisa wa ngazi ya juu wa Russia kufuatia ziara hiyo ya Rais wa Ukraine mjini Washington.

Dmitry Peskov, Msemaji wa ikulu ya Russia 

Imeelezwa kuwa, makombora na misaada hiyo ya kijeshi ya Marekani itatumika kuilinda Ukraine dhidi ya mashambulizi ya anga ya Russia ambayo kiev inadai yanalenga miundombinu ya kiraia kama mitambo ya kuzalisha umeme, na hivyo kusababisha kukatika huduma ya umeme kote nchini.

Wakati huo huo Rais Joe Biden wa Marekani ameeleza kuwa, nchi yake na Ukraine zitaendelea kudumisha ulinzi wa pamoja  kufuatia kile alichokiita hujuma za kikatili za Russia dhidi ya haki ya Ukraine ya kuendelea kuwepo kama taifa.