Jan 24, 2023 02:51 UTC
  • Kisingizio cha Sweden cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu; chuki dhidi ya Uislamu nyuma ya pazia la uhuru wa kusema

Tobias Billstrom, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sweden ameandika ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akitoa radiamali ya hatua ya mataifa mbalimbali ya dunia ya kukosoa kuvunjiwa heshima kitabu kitakatifu wa Qur'ani.

Billstrom ameandika katika ujumbe wake huo: "Uchochezi dhidi ya Uislamu ni jambo la kutisha. Sweden ina uhuru kamili wa kusema na kutoa maoni, lakini hii haina maana kwamba, serikali ya Sweden au mimi ninaunga mkono mitazamo hii."

Kwa msingi huo matamshi hayo yanaonyesha kuwa, serikali ya Sweden imeamua kushikamana na msimamo wa kindumakuwili katika kadhia ya kutusiwa na kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu tukio ambalo limetokea katika mji mkuu wa nchi hiyo Stockhom.

Jumamosi iliyopita, Rasmus Paludan kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia na mwenye chuki dhidi ya Uislamu wa Denmark, alichoma moto nakala ya kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani Tukufu nje ya ubalozi wa Uturuki katika mji mkuu wa Sweden Stockholm. Kiongozi huyo wa chama cha Stram Kurs, kwa kimombo Hard Line ambaye asili yake ni Mdenmark alipata uraia wa Sweden mwaka 2020.

Mwanasiasa huyu ni mashuhuri kwa kuwa na misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu na wahajiri.  Rasmus Paludan amewahi kushtakiwa mara kadhaa nchini Denmark kwa makosa ya kukiuka sheria. Hivi sasa ameanza kutekeleza kitendo cha kishenzi cha kuchoma Qur'ani Tukufu katika miji mbalimbali ya Sweden. Kila mji au eneo analokwenda ambalo lina wahajiri Waislamu huchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu.

Malalamiko na radiamali kali ya Waislamu wahajiri, hupelekea kuibuka vurugu baina yao na vikosi vya usalama. Kabla ya hapo, Rasmus Paludan amewahi kuwania kiti cha Ubunge nchini Denmrak mwaka 2019 ambapo nara yake katika kampeni ilikuwa "Kuisafisha Denmark na Waislamu" na "Marufukuu ya Uislamu nchini Denmrak". Hata hivyo alishindwa katika uchaguzi huo. Baada ya kupata uraia wa Sweden alitangaza kuwa, ana matumaini ya kuendesha harakati zake kwa wigo mpana zaidi nchini Sweden. Mwanaharakati huyo mwenye misimamo ya kufurutuu ada mwaka 2022 alichoma nakala moja ya Qur'ani Tukufu katika mji wa Malmo Sweden, tukio ambalo lilipelekea kuibuka malalamako na vurugu kubwa za utumiaji mabavu.

Kitendo cha Rasmus Paludan, kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia na mwenye chuki dhidi ya Uislamu wa Denmark cha kuchoma moto nakala ya kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani Tukufu nje ya ubalozi wa Uturuki katika mji mkuu wa Sweden Stockholm, kimekabiliwa na malalamiko na upinzani mkali katika maeneo mbalimbali ya dunia.

Nasser Kan'ani, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigenii wa Iran amesema, kukaririwa kitendo hicho cha kuchomwa moto Kitabu Kitukufu cha Waislamu ni mfano mwingine wa chuki dhidi ya Uislamu, na njama za kuchochea ghasia miongoni mwa wafuasi bilioni 1.5 wa dini hiyo tukufu.

Kan'ani ameeleza bayana kuwa: Kwa bahati mbaya, shakhsia wenye misimamo mikali wanaruhusiwa kufanya wanachotaka katika baadhi ya nchi za Ulaya, kwa kisingizio cha uhuru wa maoni na kujieleza. Njama hizi zinalenga kuchochea chuki dhidi ya matukufu na thamani za Uislamu.

Kwa upande wake, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Pakistan imelaani vikali uafriti huo na kusema, hatua hiyo ya kuchomwa moto Kitabu hicho Kitakatifu cha Waislamu kimeumiza hisia za Waislamu zaidi ya bilioni 1.5 kote duniani, na ni tusi dhidi ya matukufu yao.

Islamabad imesema hatua hiyo haihalalishiki kwa vyovyote, hata kwa kutumia kisingizio cha kipumbavu cha uhuru wa maoni. Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Pakistan imebainisha kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kuonyesha msimamo mmoja dhidi ya chuki dhidi ya Uislamu na dini nyinginezo, pamoja na matukufu yao.

Kabla ya hapo, Uturuki na Baraza la Ushirikiano wa Kiislamu la Sweden zilitoa taarifa ya kulaani vikali kitendo hicho cha kuchomwa moto Qur'ani Tukufu nje ya ubalozi wa Uturuki jijini Stockholm nchini Sweden.

Nukta ya kuzingatia nii hii kwamba, hata mataifa yasiyo ya Kiislamu nayo yamejitokeza na kukemea kuchomwa moto nakala ya Qur;ani tukufu.  Mikhail Ulyanov, balozi wa Russia katika asasi za kimataifa zenye makao yake mjini Vienna Austria amekosoa vikali kitendo cha kuchomwa moto Qur'ani Tukufu na kuandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba: "Kitendo hiki ni aina ya ubedui na unyama, na kinachochea mizozo baina ya dini mbalimbali.

Mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu na vitendo vya utumiajii mabavu dhidi ya wafuasi wa dini hii vimechukua wigo wa kuongezeka katika miaka ya hivi karibuni huko barani Ulaya. Kisingizo cha tawala za Denmark na Sweden cha kumruhusu Rasmus Paludan kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu kinatajwa kuwa ni uhuru wa kusema.

Hii ni katika hali ambayo, tukitupia jicho nara ya uhuru wa kusema inayopigiwa upatu na ulimwengu wa Magharibi yakiwemo mataifa ya Ulaya tunashuhudia undumakuwili na unafiki wa wazi kabisa. Ukweli wa mambo ni kuwa, uhuru wa kujieleza kwa mataifa ya Magharibi huzingatiwa na kuwa na maana pale unapoendana na matakwa yao kama kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu. Lakini kuhusiana na masuala mengine kama ngano ya Holocaust mambo ni kinyume kabisa kwani walimwengu wameshuhudia madola hayo yakichukua hatua kali dhidi ya watu wanaokana au hata kuhoji tu kuhusiana na kile kinachoelezwa kama mauaji ya kimbari ya Mayahudi katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Tags