Mar 18, 2024 02:33 UTC
  • Joe Biden akiri kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu Marekani

Ijumaa, Februari 15, Rais Joe Biden wa Marekani huku akikiri kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo tangu kuanza mashambulizi ya Wazayuni huko Gaza alisema: 'Waislamu kote duniani wanapitia hali ngumu kutokana na imani yao.'

Akizungumza katika Siku ya Kimataifa ya kupambana na chuki dhidi ya Uislamu, Biden alisema, "tunafahamu vyema chuki inayowakabili Waislamu kote ulimwenguni mara nyingi kutokana na imani zao za kidini na kuibuka chuki chafu dhidi ya Uislamu kufuatia vita vyenye uharibifu mkubwa huko Gaza." Alidai kuwa chuki dhidi ya Uislamu haina nafasi nchini Marekani. Mbali na madai hayo Waislamu wa Marekani wanakabiliwa na hali ngumu ya hofu ya kushambuliwa, ubaguzi wa wazi, unyanyasaji na vitendo vya mabavu katika maisha yao ya kila siku.

Kukiri Rais wa Marekani kuhusu ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu nchini humo hasa baada ya kuanza vita vya Gaza kunaweza kutathminiwa katika mtazamo wa matukio yanayotokea kila siku katika nchi hiyo dhidi ya Waislamu. Bila shaka chuki dhidi ya Uislamu iliongezeka kwa kasi katika kipindi cha utawala wa Donald Trump, rais wa zamani wa nchi hiyo, ambaye ana mitazamo mikali ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Mashirika ya haki za binadamu yamelinganisha kuenea chuki dhidi ya Uislamu baada ya operesheni ya kimbunga cha al-Aqsa mnamo Oktoba 7 na tuhuma dhidi ya Waislamu baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani. Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu limetangaza kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho ya 2023, malalamiko 578 kuhusu chuki dhidi ya Waislamu na Wapalestina yaliripotiwa. Idadi hiyo iliongezeka kwa asilimia 178 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.

Chuki dhidi ya Uislamu

Moja ya vitendo vya wazi na vya kikatili vya chuki dhidi ya Waislamu baada ya vita vya Gaza ni mauaji ya mtoto wa Kipalestina aliyekuwa na umri wa miaka 6 na kujeruhiwa mama yake na Mmarekani mwenye chuki kali za mrengo wa kulia katika jimbo la Illinois katikati ya mwezi Oktoba 2023, wiki moja baada ya kuanza vita hivyo. Kwa mujibu wa polisi, mtoto huyo wa kiume alidungwa kisu mara 26 nyumbani kwao Plainfield na katili huyo Joseph Chuba mwenye umri wa miaka 71 na kufariki akiwa hospitalini. Mama yake mwenye umri wa miaka 32 pia alidungwa kisu mara kadhaa. Katili huyo ni muungaji mkono mkubwa wa utawala wa Kizayuni. Kitendo hicho cha jinai kilikuwa cha kinyama kiasi kwamba hata Ikulu ya White House ililazimika kukilaani.

Jinai hiyo kubwa dhidi ya mama na mtoto wake Waislamu huko Chicago ilitokea kutokana na kuongezeka anga ya chuki dhidi ya Waislamu wa Marekani katika kivuli cha vita kati ya utawala wa Kizayuni na makundi ya muqawama ya Palestina. Jinai hiyo inaonyesha kuenea kwa misimamo mikali na ukatili wa kibaguzi unaosababishwa na chuki hususan dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Marekani. Kuhusiana na hilo, Christopher Ray, Mkurugenzi wa FBI, ameonya kuhusu ongezeko hilo la chuki kali na kusema: 'Hakuna shaka kwamba vitisho vinaongezeka.'

Kwa kuzingatia mwenendo unaoongezeka wa vitisho na chuki dhidi ya Waislamu nchini Marekani, Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Marekani limetoa wito wa kukomeshwa chuki dhidi ya Uislamu na Palestina miongoni mwa wanasiasa na vyombo vya habari vya Marekani. Chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu huko Marekani, ilianza kupata kasi baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001, na kufikia kilele wakati wa urais wa Donald Trump, ambaye ana chuki ya wazi dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Hivi sasa ubaguzi na unyanyasaji wa kimwili na wa maneno dhidi ya Waislamu wa Marekani umeongezeka kutokana na kuimarika makundi ya mrengo wa kulia na vilevile vita vya propaganda na vyombo vya habari dhidi ya Waislamu hususan baada ya matukio ya hivi karibuni katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Chuki hiyo inatekelezwa kupitia mambo kama vile mashambulizi ya kikatili dhidi ya Waislamu, hasa wale wanaofanana na watu wa nchi za Kiislamu za Asia Magharibi, kuchoma moto maeneo ya ibada ya Waislamu, mashambulizi ya maneno na vitisho dhidi yao na kuongezeka chuki dhidi ya Waislamu katika vyombo vya habari vya Marekani.

Tags