Jan 29, 2023 07:23 UTC
  • Waislamu Uingereza waandamana kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu

Waislamu wa Uingereza wamekusanyika mbele ya uubalozi wa Sweden mjini London wakilaani kitendo kiovu cha nchi hiyo ya Ulaya cha kuruhusu kudhalilishwa na kuvunjiwa heshika kitabu kitakatifu cha Qur'ani.

Ni baada ya vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu siku za Jumamosi iliyopita nchini Uswidi ambapo watu wenye misimamo mikali walivunjia heshima na kuchoma moto nakala ya Qur’ani Tukufu mbele ya Ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm, katika kitendo ambacho kiliidhinishwa na kusimamiwa na polisi wa Sweden.

Makumi ya Waislamu wa Uingereza jana walifanya maandamano mbele ya ubalozi wa Uswidi, wakiwa wamebeba mabango na yenye maandishi yanayolaani kitendo cha nchi hiyo cha kudhalilisha Qur'ani Tukufu na kuwalaumu viongozi na waliohusika na hujuma hiyo dhidi ya matukufu ya Waislamu karibu bilioni mbili kote duniani.

Katika maandamano hayo, Waislamu waliokusanyika kutoka miji tofauti ya Uingereza walisoma Aya za Qur'ani Tukufu baada ya kuswali Swala ya Adhuhuri kwa jamaa.

Kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu kumezusha wimbi la hasira na malalamiko makali ya Waislamu kote duniani, na watetezi wa uhuru wa itikadi pia wamelaani vikali kuchomwa moto nakala ya kitabu hicho kitakatifu.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki, Misri, Kuwait, Umoja wa Falme za Kiarabu, taasisi ya Al-Azhar nchini Misri, Baraza la Wanazuoni wa Kiislamu Duniani, Qatar, Saudi Arabia, Indonesia, Jordan, Morocco, Mauritania, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Hamas na harakati ya Jihad ya Kiislamu ya Palestina ni miongoni mwa nchi na taasisi zilizochukua msimamo mkali dhidi ya kitendo hicho cha kuchukiza na kutoa wito wa kuadhibiwa wahusika.

Ijumaa ya wiki hii pia mamilioni ya Waislamu wa Iran walifanya maandamana baada ya Swala ya Ijumaa kote nchini wakilaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya.

Tags