Mamia wapoteza maisha katika mtetemeko mkubwa wa ardhi Uturuki, Syria + Video
(last modified Mon, 06 Feb 2023 08:06:55 GMT )
Feb 06, 2023 08:06 UTC

Mtemtemeko mkubwa wa ardhi umetikisa maeneo ya kusini mashariki mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria na kuua watu wasiopungua 400 huku idadi ya waliopoteza maisha ikitazamiwa kuongezeka.

Kwa mujibu wa taarifa mtetemeko huo uliokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha rishta ulijiri saa kumi na dakika 17 alfajiri kwa saa za eneo hilo ambapo kitovu chake kilikuwa katika miji ya Uturuki ya Gaziantep ambapo majengo kadhaa yameporomoka.

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ametuma ujumbe katika ukurasa wa Twitter na kusema timu za uokoaji zilitumwa mara moja katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko hilo.

Nchini Syria idadi kubwa ya watu wamefariki na wengine wengi kujeruhiwa katika miji ya Aleppo, Latakia na Hama.

Raed Ahmed ambaye ni mkuu wa Kituo cha Kitaifa cha Zilzala Syria amesema mtetemeko huo ni mkubwa zaidi kuwahi kurekodiwa na kituo hicho. Mitetemeko midogo pia imehisika katika nchi za karibu kama vile Lebanon na Cyprus.

Uturuki ni miongoni mwa nchi ambazo hukumbwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi mara kwa mara duniani. Mwaka 1999 watu 18,000 walipoteza maisha katika mtetemeko mkubwa wa ardhi kuwahi kuikumba nchi hiyo kwa miongo kadhaa.