Lukashenko: Belarus itaungana na Russia katika vita vya Ukraine ikishambuliwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i94132-lukashenko_belarus_itaungana_na_russia_katika_vita_vya_ukraine_ikishambuliwa
Rais Alexander Lukashenko wa Belarus ameonya kuwa, iwapo nchi hiyo itashambuliwa, basi haitakuwa na budi kuungana na Russia katika vita dhidi ya Ukraine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 16, 2023 23:19 UTC
  • Lukashenko: Belarus itaungana na Russia katika vita vya Ukraine ikishambuliwa

Rais Alexander Lukashenko wa Belarus ameonya kuwa, iwapo nchi hiyo itashambuliwa, basi haitakuwa na budi kuungana na Russia katika vita dhidi ya Ukraine.

Rais Lukashenko alisema hayo jana Alkhamisi na kufafanua kuwa, iwapo nchi hiyo ya Ulaya Mashariki itashambuliwa, itajiunga na safu ya mapambano ya kijeshi na Russia katika vita vya Ukraine.

Sanjari na kuilaumu Kiev kwa vita vinavyoendelea Ukraine, Rais wa Belarus ameeleza bayana kuwa, nchi za Ulaya hazitaki vita na Belarus, lakini Marekani inafanya juu chini kuona nchi hiyo inatumbukia katika mgogoro na mapigano.

Kauli ya Lukashenko inakuja baada ya Katibu Mkuu wa shirika la kijeshi la NATO, Jens Stoltenberg kusema kuna uwezekano wa Finland na Sweden kujiunga na shirika hilo la kijeshi la nchi za Magharibi katika mwaka huu wa 2023.

Rais Lukashenko (kulia) na Rais Vladimir Putin wa Russia

Huko nyuma pia, Rais Lukashenko alisema Washington imeazimia kuanzisha vita nchini Belarus kwa kuyatumia mataifa ya Poland, Ukraine na nchi za eneo la Baltic.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa, lengo la nchi za Magharibi ni kumng'oa madarakani Rais Alexander Lukashenko, ili kupandikiza mtu mwenye mielekeo ya Kimagharibi na adui wa Russia.