Feb 24, 2023 03:06 UTC
  • Hungary yailaumu Marekani kwa 'kuididimiza' Ulaya

Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orbán ameilaumu Marekani kwa kusababisha kudidimia na kupoteza ushawishi nchi za Ulaya.

Gazeti la Magyar Nemzet limemnukuu Orbán akisema hayo katika hotuba yake mbele ya wanachama wa muungano tawala wa Fidesz-KDNP na kuongeza kuwa, sera za Rais Joe Biden wa Marekani zimechangia kuporomoka Ulaya.

Orbán amesema: Ulaya imedhoofika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kwa sababu utawala wa Biden unang'ang'ania maslahi yake bila mipaka huko Brussels, huku ukipuuza maslahi ya bara Ulaya. 

Waziri Mkuu wa Hungary amesema wimbi la vikwazo dhidi ya Russia kama jibu kwa mgogoro wa Ukraine limeutia kwenye matatizo mengi uchumi wa nchi za Ulaya, huku Marekani ambayo ina nishati ya kutosha ya bei rahisi ikiwa mbali na changamoto hizi (zinazopitia nchi za Ulaya).

Mgogoro wa nishati Ulaya

Hivi sasa nchi za Ulaya zinaendelea kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa nishati baada ya nchi za bara hilo kuiwekea vikwazo Russia kwa kisingizio cha vita vya Ukraine.

Mwaka jana, Orbán mara kadhaa amemlaumu Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kwa kukubali kuchochewa na nchi za Magharibi na kuitumbukiza nchi yake kwenye vita angamizi na Russia.

Tags