Watu wenye silaha watishia kumuua nyota wa soka duniani Lionel Messi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i94664-watu_wenye_silaha_watishia_kumuua_nyota_wa_soka_duniani_lionel_messi
Watu wawili wenye silaha wamefyatua risasi zisizopungua kumi na kuacha ujumbe wa vitisho kwa nyota wa soka wa Argentina Lionel Messi katika uvamizi wa duka kubwa linalomilikiwa na wakwe zake mjini Rosario, Argentina. Maafisa wa vyombo vya mahakama wa mji huo wamelielezea tukio hilo lililotokea Alkhamisi asubuhi kuwa ni la kigaidi.
(last modified 2025-12-03T16:38:35+00:00 )
Mar 03, 2023 07:01 UTC
  • Watu wenye silaha watishia kumuua nyota wa soka duniani Lionel Messi

Watu wawili wenye silaha wamefyatua risasi zisizopungua kumi na kuacha ujumbe wa vitisho kwa nyota wa soka wa Argentina Lionel Messi katika uvamizi wa duka kubwa linalomilikiwa na wakwe zake mjini Rosario, Argentina. Maafisa wa vyombo vya mahakama wa mji huo wamelielezea tukio hilo lililotokea Alkhamisi asubuhi kuwa ni la kigaidi.

Polisi imesema, shambulio hilo lilitokea katika duka kubwa la Unico linalomilikiwa na familia ya mke wa Messi, Antonella Roccuzzo, katika mji wa Rosario. Washambuliaji hao wawili walifika dukani hapo wakiwa wamepanda pikipiki na kufyatua risasi zisizopungua 12 kuelekea duka hilo.

Sambamba na shambulio hilo, watu hao waliacha pia ujumbe wa maandishi kwa mwanasoka huyo wa kulipwa kwenye kipande cha kadibodi kwenye duka hilo, unaosomeka "Messi, tunakusubiri." Ujumbe huo umemlenga pia mwanasiasa wa eneo hilo, Meya wa Rosario Pablo Javkin, ukidai kuwa yeye ni "mfanyamagendo wa dawa za kulevya" na "hangemtunza" Messi.

Lionel Messi na ujumbe wa kutishia kumuua aliotumiwa

Afisa wa vyombo vya mahakama, mwendesha mashtaka Federico Rebola amesema hakukuwa na aliyejeruhiwa katika ufyatuaji risasi huo, ambao ulikuja huku kukiwa na ongezeko la ghasia zilizohusishwa na makundi ya wahalifu katika mji huo wa Rosario.

Waziri wa Sheria wa jimbo la Santa Fe, Celia Arena, ameutaja ufyatuaji risasi huo kuwa ni kitendo cha "kigaidi" kilichotekelezwa na shirika la "mafia".

Messi, ambaye ana nyumba huko Rosario na hutembelea familia mara kwa mara huko, hadi sasa hajatoa kauli yoyote juu ya tukio hilo.

Akiwa anatambuliwa kama mmoja wa wanasoka bora zaidi wa zama zote, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 alishinda tuzo ya mchezaji bora wa kiume wa FIFA mapema wiki hii mbali na kuiongoza timu ya taifa ya Argentina na kutwaa kombe la dunia katika mashindano yaliyofanyika mwaka jana nchini Qatar baada ya kushindwa kulinyakua kombe hilo kwa miongo kadhaa.../