Kukiri Washington woga wa Marekani wa kubadilika mfumo wa dunia
Taasisi za kijasusi za Marekani zimetoa ripoti yao ya pamoja ya kila mwaka kuhusu vitisho vilivyoko duniani na kuelezea wasiwasi wake mkubwa wa kubadilika mfumo wa utawala wa dunia hasa kutoka kwa nchi kama China.
Sehemu moja ya ripoti hiyo imesema, mwaka ujaoMarekani na waitifaki wake watakumbwa na kipindi kigumu katika masuala ya usalama. Anga ya kipindi hicho itatawaliwa na changamoto mbili kuu za kiistratijia na muhimu mno ambazo zinakinzana na zinaweza kuleta mabadiliko yasiyo ya kawaida ya kiusalama.
Changamoto ya kwanza kubwa zaidi ni madola makubwa kieneo na kimataifa ambayo yanazidi kuchipua huku taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali nayo yakizidi kushindana kutafuta udhibiti wa mambo ulimwenguni kwa ajili ya miongo mingi ijayo. Pili ni changamoto za pamoja duniani kama vile mabadiliko ya tabianchi, usalama wa mwanadamu na masuala ya afya. Hivi sasa dunia bado inauguza majeraha ya janga la UVIKO-19 yaani corona ambalo limeathiri vibaya uchumi na kuhatarisha usalama wa chakula duniani.
Hatua ya Marekani ya kutangaza waziwazi hofu yake kuhusu kutokea mabadiliko ya kimsingi katika mfumo wa utawala duniani wakati huu wa baada ya vita baridi, inatokana na kujitokeza madola mapya yenye nguvu duniani hasa China pamoja na kuzidi kupata nguvu nchi kama Russia. Mfano wa wazi wa mabadiliko hayo ya kimsingi katika mfumo wa utawala wa dunia, ni kupungua pole pole ushawishi wa kundi la G20 linaloundwa na nchi zenye nguvu za kiuchumi duniani na nchi zenye uchumi unaostawi kwa kasi. Hilo pekee ni ushahidi wa kutoka udhibiti wa kiuchumi mikononi mwa madola ya Magharibi na kuzuka madola mapya yenye nguvu za kiuchumi kieneo na kimataifa.
Hivi sasa wapinzani wakubwa wa nchi za Magharibi yaani China na Russia zina ushirikiano mzuri na madola makubwa mapya ya kiuchumi kama Afrika Kusini, Brazil na India ambayo kwa pamoja yameunda kundi lenye nguvu la BRICS. Hii ina maana kwamba ndoto za Marekani za kuona dunia inatawaliwa na kambi moja inayoongozwa na Washington, ni mustahili kuaguka.
China na Russia zinaamini kuwa, matukio yanayotokea hivi sasa ni uthibitisho kuwa dunia sasa hivi imenza kuingia kikwelikweli kwenye mfumo wa kambi kadhaa. Lakini Marekani ingali inashikilia ndoto zake za kuweko mfumo wa kambi moja tu duniani na inaendelea kujifanya polisi wa dunia. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana kambi ya Magharibi inayoongozwa na Marekani inahamakishwa mno na ushirikiano unaozidi kukua baina ya Russia na China. Marekani ina wahka mkubwa wa kuona ushawishi wa China na Russia unazidi kuwa mkubwa kieneo na kimataifa ndio maana inafanya njama za kila namna kujaribu kuonesha kuwa, nchi hizo mbili ni tishio kwa usalama wa dunia. Maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi na kiusalama wa serikali ya Joe Biden, mara chungu nzima wamesikika wakisema, changamoto kubwa zaidi ya jeopolitiki kwa Marekani ni China na Russia na wanadai kuwa madola hayo mawili yanatishia uwepo wa mfumo wa utawala wa kimataifa unaotegemea uliberali. Maafisa hao wa Biden wanadai pia kuwa Russia ni tishio kubwa kwa Marekani na waitifaki wake na ndio maana wanafanya kila njia kuhakikisha Russia haiibuki mshindi katika vita vya Ukraine. Sehemu moja ya ripoti mpya ya mashirika ya kijasusi ya Marekani imesema, ushindani wa kimkakati baina ya Marekani na waitifaki wake kwa upande mmoja na China na Russia kwa upande wa pili, unatokana na namna mfumo wa utawala duniani unavyopaswa kuwa na hilo ni muhimu mno kwa nchi za Magharibi.
Inavyoonekana ni kuwa, wahka mkubwa wa Marekani unatokana na kushindwa kwake kukabiliana na kasi ya ushawishi na nguvu za China ambayo leo inahesabiwa ni dola lenye uchumi mkubwa zaidi duniani. Mashirika ya kijasusi ya Marekani yamesema katika ripoti yao kuwa, China ina uwezo wa kutosha wa kufanya mabadiliko yoyote ya moja kwa moja katika nyuga na maeneo yote duniani.
Avril Danica Haiens, mkuu wa usalama wa taifa wa Marekani alipohotubia kikao cha masuala ya kijasusi cha Baraza la Sanate la Marekani, mbali na kukiri kwamba China hivi sasa haitaki kuongeza mivutano na Marekani na inafadhilisha kuwa na uhusiano wenye utulivu kati yake na Washington, alisema, China inatoa changamoto kubwa kwa Marekani kote ulimwengu katika upande wa uchumi, tekonolojia pamoja na masuala ya kisiasa na kijeshi na itaendelea kuwa kipaumbele kisicho na mbadala kwa Marekani.