Mar 19, 2023 05:52 UTC
  • Vyombo vya usalama vya Marekani vyajitayarisha kumkamata rais wa zamani wa nchi hiyo, Trump

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa askari usalama wa Marekani wanajitayarisha kwa ajili ya kumkamata rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump kuhusiana na faili la uhalifu lililofikishwa mahakamani.

Tovuti ya RT imeripoti kwamba, askari usalama wa Marekani wanajiandaa kwa uwezekano wa kukamatwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump.

Ripoti hiyo imesema, vyombo vya sheria vya serikali ya Federali, majimbo na serikali za mitaa vinajadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu kiwango cha utayarifu na usalama iwapo Donald Trump atafunguliwa mashtaka ya kughushi na kutoa ushahidi wa uongo katika siku zijazo.

Maafisa watano wa ngazi za juu wa Marekani wamesema mashirika ya usalama yanafanya "tathmini ya awali ya usalama" katika eneo la Manhattan juu ya uwezekano wa kufunguliwa mashtaka Donald Trump kuhusiana na kesi ya kutoa hongo inayohusisha mwanamke aliyedai kuwa na uhusiano wa kingono na rais huyo wa zamani wa Marekani.

Trump pia anahusika katika uchunguzi ulioanzishwa na Ofisi ya Mwanasheria wa Wilaya ya Manhattan kwa madai ya kughushi rekodi za biashara.

Trump anatuhumiwa kumpatia dola 130,000 mwigizaji wa filamu za ponografia, Stormy Daniels, kupitia kwa wakili wake, Michael Cohen.

Stormy Daniels akiwa pamoja na Trump

Daniels anadai kwamba, wakati wa kampeni ya uchaguzi wa rais wa Marekani 2016 alilipwa pesa ili kukaa kimya kuhusu madai ya uhusiano wake wa kingono na Donald Trump.

Shirika la habari la Reuters pia limetangaza kwamba, Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani, amedai kwamba atakamatwa siku ya Jumanne, Machi 21 kuhusiana na faili la kesi yake iliyoko mahakamanina na kutoa wito kwa wafuasi wake kupinga hatua hiyo kwa kuandamana. Ujumbe wa Trump katika jukwaa la mtandao wa kijamii la Truth Social unatajwa kuwa una lengo la kuzusha wimbi jingine la machafuko na mivutano nchini Marekani. 

Tags