Kuendelea utunishaji misuli na ubabe wa China mbele ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i96238-kuendelea_utunishaji_misuli_na_ubabe_wa_china_mbele_ya_marekani
Ijapokuwa China ilitangaza hivi majuzi kuwa mazoezi yake ya kijeshi ya pande zote iliyofanya kwa mfananisho wa kukizingira kisiwa cha Taiwan yamemalizika, lakini televisheni ya taifa ya nchi hiyo ilitangaza kuwa, manowari kadhaa za Beijing zitaendelea kutoa mafunzo yanayohitajika kuendana na uhalisia wa hali ya vita katika maji yanayoizunguka Taiwan ili kupima uwezo wake katika ngazi zote na ufanisi wa silaha na zana zake za kivita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 13, 2023 22:43 UTC
  • Kuendelea utunishaji misuli na ubabe wa China mbele ya Marekani

Ijapokuwa China ilitangaza hivi majuzi kuwa mazoezi yake ya kijeshi ya pande zote iliyofanya kwa mfananisho wa kukizingira kisiwa cha Taiwan yamemalizika, lakini televisheni ya taifa ya nchi hiyo ilitangaza kuwa, manowari kadhaa za Beijing zitaendelea kutoa mafunzo yanayohitajika kuendana na uhalisia wa hali ya vita katika maji yanayoizunguka Taiwan ili kupima uwezo wake katika ngazi zote na ufanisi wa silaha na zana zake za kivita.

Hatua hiyo ya jeshi la China iliyochukuliwa baada ya kuanza mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya Marekani na Ufilipino katika Bahari ya China Kusini inaonyesha wazi kuwa Beijing inaendelea kutunisha misuli na kuonyesha ubabe mbele ya Marekani. China inaichukulia Taiwan kama sehemu isiyotenganika na ardhi yake na imeshaitaka Marekani mara kadhaa ikomeshe chokochoko inazofanya kuhusiana na suala hilo. Hata hivyo, Marekani imeonyesha kuwa dhamira yake ni kuzidisha mashinikizo kwa China, kwa kuunga mkono harakati za Taiwan za kutaka kuwa huru na kujitawala, kwa kufanya manuva na mazoezi ya pamoja ya kijeshi na washirika wake katika maeneo ya kandokando ya China.

Kuhusiana na hilo, Abolfazl Zahrevand, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema: "Marekani inaichukulia China sio tu mshindani wake mkubwa katika nyanja za uchumi na teknolojia, lakini kwa kuongezeka kila uchao nguvu za China, inahisi mamlaka yake kimataifa yanakabiliwa na hatari kubwa. Kwa sababu hii, kuanzia kipindi cha uongozi wa rais aliyepita Donald Trump, Marekani ilichochea vita vya kibiashara baina yake na China na kushadidisha uungaji mkono wake kwa wanaopigania kujitawala Taiwan ili kuishughulisha zaidi Beijing na masuala yake ya ndani".

 
Hata hivyo, kwa kuimarisha kuwepo kwake kijeshi katika eneo la majini linaloizunguka Taiwan, China imeionyesha Marekani kuwa haitaruhusu kivyovyote vile nchi za Magharibi na hasa Washington ivuke mstari mwekundu wa Beijing kuhusiana na Taiwan. Mazoezi ya hivi karibuni ya jeshi la China ya kuigiza namna ya kuizingira Taiwan na kuendelea kuwepo meli za kivita za China kandokando ya kisiwa hicho kwa ajili ya kufanya operesheni za doria vimefikisha ujumbe wa wazi kwa Marekani kwamba China haitalegeza kamba kwa namna yoyote ile katika kanuni na misingi yake mikuu; na kufanya Washington mazoezi ya kijeshi na muitifaki wake yeyote wa kijeshi ikiwemo Ufilipino hakuwezi kuitia hofu Beijing au kuupa matumaini mrengo unaounga mkono kujitawala Taiwan kwamba utaweza kujitenga na ardhi ya asili ya China.
Henry Kissinger

Henry Kissinger, mwanadiplomasia mkongwe wa Marekani na mchambuzi wa masuala ya kimataifa, ameionya mara nyingi Washington kuhusu matokeo hatari ya kumalizika stahamala na uvumilivu wa China kuhusiana na Taiwan. Kwa mtazamo wa Kissinger, China imeonyesha kuwa haiko tayari katu kulegeza kamba na kurudi nyuma kuhusiana na Taiwan, na kuongezeka mashinikizo ya Marekani katika suala hilo kunaweza kukawa na matokeo yasiyoweza kutabirika.

 
Kwa vyovyote vile, maandamano ya watu wa Manila mji mkuu wa Ufilipino ya kupinga mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya nchi yao na Marekani yanaonyesha kuwa hali kiujumla katika eneo hilo haiendani na maslahi ya Marekani, na watu katika nchi waitifaki wa Washington nao pia wana wasiwasi kuhusu matokeo ya sera za Washington za kushupalia vita. Wakati huo huo, nchi washirika wa Marekani zinapaswa kuzingatia ukweli kwamba endapo utazuka mgogoro wowote katika Mlango-Bahari wa Taiwan; na Marekani ikaamua kutumia vituo vyake vya kijeshi katika eneo hilo, ni nchi hizo wenyeji wa majeshi ya Marekani ndizo zitakazopata madhara na hasara kubwa zaidi endapo China itachukua hatua ya kufanya mashambulio ya kujibu mapigo.
 
 
Lakini mbali na hayo, nchi za eneo hilo zinategemea zaidi usafirishaji wa bidhaa nje, na kwa hivyo kuongezeka mivutano katika Bahari ya China Kusini kunaweza kuwa na athari mbaya na hasi kwa hali ya kiuchumi ya nchi za eneo hilo, zikiwemo Japan na Korea Kusini. Kwa hiyo, haionekani kama nchi za eneo hilo zitapuuza maonyo na indhari za China na kuyakaribisha madola ajinabi na ya kigeni kwenye eneo la maji yanayoizunguka China na kudhani kwamba zitakuwa salama zitakapokuwa chini ya bendera ya Marekani.../