Kugombea kwa "Joe Biden" katika uchaguzi wa 2024 na changamoto zinazomkabili
Hatimaye baada ya tetesi za muda mrefu, Rais wa Marekani, Joe Biden ametangaza rasmi kuwa atagombea katika uchaguzi wa rais wa 2024, na iwapo atashinda, atabaki katika Ikulu ya White House kwa miaka mingine minne.
Biden na wafuasi wake wanatumai kuwa watashinda tena katika uchaguzi wa Novemba 5, 2024 na kuidhibiti tena Ikulu ya White House. Hii ni licha ya kwamba asilimia 26 tu ya watu wa Marekani tu ndio wanaokubalina na hatua ya Biden ya kutangaza nia yake ya kugombea tena katika uchaguzi ujao wa urais wa nchini humo.
Katika video iliyosambazwa kwa umma, Biden, amewaomba wapiga kura wampe muda zaidi wa "kukamilisha kazi" aliyoahidi mwanzoni mwa urais wake na kutupilia mbali wasiwasi wao kuhusu kuongezwa muda wa rais huyo mzee zaidi wa Marekani kwa miaka mingine minne.
Kwa upande mwingine, kuna uwezekano mkubwa kwamba "Donald Trump" atakuwa mpinzani mkuu wa Biden katika uchaguzi huo. Trump alitangaza nia yake ya kugombea katika uchaguzi ujao muda mrefu uliopita na alitoa ahadi za kuboresha hali ya Marekani.
Uchaguzi ujao nchini Marekani unaandamana na changamoto nyingi. Ongezeko la bei ya bidhaa mbalimbali, athari hasi za vita vya Ukraine na ushiriki wa Marekani katika vita hivyo, kushadidi mivutano ndani ya Marekani na kuondoka bila mpango na kiholela kwa wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan ni miongoni mwa mambo yanayonyooshewa kidole na wapinzani wa Biden kama sababu za kupinga ushiriki wake kama mgombea katika uchaguzi ujao.
Kwa upande mwingine, katika miezi ya hivi karibuni, Biden amekosolewa na raia wengi wa nchi hiyo kutokana na hali yake ya kiakili na kiafya. Seneta Tim Scott anaonya kuhusiana na jambo hili akisema: "Usimamizi wa uchumi wa Biden unaharibu mustakabali wa kiuchumi wa familia za Marekani."
Hata hivyo, wafuasi wa Biden wamekuwa wakizungumzia na kumulika mafanikio ya utawala wake. Wafuasi hao wanadai kuwa, mafanikio makubwa ya utawala wa Biden katika chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19, ambayo hatimaye yalipelekea kupungua maambukizo na vifo vinavyosababishwa na virusi vya corona, koboreka kiasi kwa uchumi wa Marekani na kupunguza ukosefu wa ajira nchini humo, ni miongoni mwa mafanikio ya Joe Biden.
Pamoja na hayo, kura za maoni zinaonyesha kuwa, wapiga kura wengi wa Marekani wanataka kuwekwa kando Joe Biden na Donald Trump na kuzuiwa kugombea katika uchaguzi ujao, na hawataki wawili hao wachuane tena katika kinyang’anyiro hicho.
Kura ya maoni iliyofanywa hivi karibuni na Yahoo News inaonyesha kuwa, wapiga kura wa Marekani hawataki kabisa kuona Rais wa sasa Joe Biden na mtangulizi wake, Donald Trump wakigombea tena katika uchaguzi wa 2024.
Trump ambaye ametangaza nia yake ya kugombea tena katika uchaguzi ujao wa rais anakabiliwa na tuhuma za kuwa na uhusiano haramu na nyota wa filamu za ngono, Stormy Daniels, na kwamba alimpa dola laki moja na elfu 30 kama kizibamdomo kabla ya uchaguzi wa rais wa 2016. Kesi hiyo inachunguzwa na waendesha mashtaka wa Mahakama ya Manhattan huko New York.
Seneta wa kujitegemea wa Marekani, Bernie Sanders, anasema: "Kitu cha mwisho ambacho nchi hii inahitaji ni Donald Trump au mtu mwingine wa mrengo wa kulia anayejaribu kudhoofisha demokrasia ya Marekani au kuondoa haki ya wanawake ya kuchagua, au kuzuia hatua yoyote ya kushughulikia mgogoro wa ukatili wa bunduki, au ubaguzi wa rangi na kijinsia."
Kwa vyovyote vile, uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2024 unaandamana na changamoto nyingi za kiuchumi na kisiasa, na kuna uwezekano kwamba matukio ya vurugu yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa urais wa 2020 yatarudiwa au hata kushadidi zaidi katika uchaguzi wa 2024.