Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuongezeka wakimbizi duniani
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limetoa ripoti mpya sambamba na kuadhimishwa Siku ya Wakimbizi Duniani na kutangaza kuwa hadi mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2015 idadi ya wakimbizi ilikuwa zaidi ya watu milioni 65.
Idadi ya wakimbizi katika mwaka 2015 ilikuwa na ongezeko la zaidi ya watu milioni tano na laki nane kulinganisha na mwaka 2014. Mapigano ya silaha na mivutano ya ndani ni sababu mbili kuu za ongezeko la idadi ya wakimbizi ambalo halijawahi kushuhudiwa; na hisia za kisiasa dhidi ya wahajiri nazo pia zimezorotesha mwenendo wa kuwapatia makazi wakimbizi katika nchi wanazokimbilia.
Wachambuzi wengi walikuwa wakifikiri kwamba baada ya kumalizika enzi za Vita Baridi (Cold War) mizozo ya kimataifa ambayo kwa mtazamo wao ilitokana na mikwaruzano kati ya Marekani na Urusi ya zamani ingepungua kwa kiwango kikubwa, lakini hali halisi inaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka 25 iliyopita tangu kusambaratika Shirikisho la Kisovieti la Urusi mapigano ya ndani na mizozo na migogoro ya kieneo imeendelea kushuhudiwa duniani.
Ukiachilia mbali sababu tofauti za kutokea migogoro, mapigano na vita, lakini yote hayo yanaunganishwa pamoja na kadhia moja ambayo hivi sasa imekuwa na wigo mpana kimataifa. Kadhia hiyo ni ya wimbi la makumi ya mamilioni ya wakimbizi kutoka nchi na pembe mbalimbali za dunia. Bila ya shaka baa la wimbi la wakimbizi, ambao wengi wao hutaabika kutafuta hifadhi baada ya kuzihama nchi zao na hasa kutaka kuelekea maeneo yenye amani barani Ulaya, sasa limekuwa na sura na hali ambayo haijawahi kushuhudiwa hapo kabla. Kwa sababu ya hali hiyo, kuna udharura wa kuwepo ushirikiano kimataifa wa kuwapatia huduma zinazostahiki watu wanaotafuta hifadhi na vilevile kuwaandalia mazingira mwafaka ya kurejea katika nchi zao.
Hata hivyo tunachoshuhudia hivi sasa ni kukosekana uratibu; na zaidi ya hayo ni kukataa kuwapokea na kuwashughulikia wakimbizi, nchi ambazo zenyewe zilichangia kuzuka machafuko na mapigano yaliyosababisha kadhia ya wimbi la wakimbizi duniani. Mfano hai wa suala hili ni wimbi la wakimbizi kutoka Mashariki ya Kati na Afrika ambao ili kuepuka machafuko na mauaji katika nchi zao wanakimbilia Ulaya kupitia Uturuki na Bahari ya Mediterania. Idadi ya wakimbizi hao katika mwaka uliopita wa 2015 ilipindukia milioni moja na laki mbili na kuufanya Umoja wa Ulaya ukabiliwe na janga linaloelezwa kuwa ni changamoto kubwa zaidi kuwahi kuukumba umoja huo tangu kuasisiwa kwake. Ukweli ni kwamba namna ya kuamiliana na wakimbizi, sasa imegeuka kuwa changamoto mpya kwa EU na kuwa moja ya sababu ya kuzuka hitilafu na mpasuko kati ya wanachama wa umoja huo. Suala hilo limekabiliwa na jibu na radiamali kali za mashirika ya kutetea haki za binadamu likiwemo Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International). Kupitia taarifa liliyotoa mwezi Juni mwaka jana, shirika hilo liliwalaumu viongozi wa nchi za Magharibi kwa kuamiliana isivyostahki na mamilioni ya wakimbizi na kutaka yawepo mashirikiano ya karibu baina ya nchi duniani kwa ajili ya kulitatua tatizo kubwa la wakimbizi. Ukweli ni kwamba hali iliyopo, ambayo imesababishwa na mamilioni ya watu kuwa wakimbizi inahesabiwa kuwa janga kubwa zaidi kushuhudiwa duniani tangu baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Pamoja na hayo inapasa tukiri kwamba kama Jamii ya Kimataifa haitokuwa na uelewa sahihi kuhusu baa la wakimbizi na kulichukulia kuwa tatizo la ulimwengu mzima, haitowezekana kupata njia na mbinu mwafaka za kulishinda tatizo hilo.../