Onyo la Pakistan kwa kundi la Taliban la Afghanistan
(last modified Wed, 31 May 2023 01:19:16 GMT )
May 31, 2023 01:19 UTC
  • Onyo la Pakistan kwa kundi la Taliban la Afghanistan

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Pakistan ameionya serikali ya wanamgambo wa Taliban wa Afghanistan kuhusiana na shambulio lolote dhidi ya ardhi ya Pakistan.

Bilawal Bhutto Zardari amesema hayo katika kikao cha kamati ya mahusiano ya kigeni ya Bunge la Seneti la Pakistan na kubainisha kwamba,  kama vitisho vya kigaidi vya serikali ya Taliban nchini Afghanistan na duniani kwa ujumla havitapewa umuhimu, basi hilo litafuatiwa na matukio ya majanga.

Zardari sambamba na kuitaka serikali ya Taliban ikabiliane na kundi la kigaidi la Takhrik-e Taliban Pakistan (TPP) amesisitiza kwanmba, hadi sasa magaidi wamefanya makumi ya mashambulio katika maeneo mbalimbali ya Pakistan na huu ndio wasiwasi mkuu wa Islamabad.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ambapo wanamgambo wa Taliban walifanikiwa kuingia tena madarakani nchini Afghanistan moja ya changamoto muhimu za wanamgambo hao na serikali ya Pakistan ni kuweko wapiganaji wa kundi la kigaidi la Tahrik-e Taliban Pakistan katika ardhi ya Afghanistan na kutumiwa ardhi ya nchi hiyo kwa ajili ya kufanya hujuma na mashambulio katika ardhi ya Pakistan. Hadi sasa mashambulio ya wanamgambo hao yamesabisha mauaji ya watu wengi nchini Pakistan.

Hatua ya Taliban ya kupuuza wasiwasi huo wa Pakistan ambayo inatathminiwa na Islamabad kwamba, ni aina fulani ya kulikirimu kundi hilo kumelifanya jeshi la Pakistan kufikia hatua ya kutishia kushambuulia ardhi ya Pakistan.  Pamoja na hayo inaonekana kuwa, serikali ya Taliban inatumia kadhia ya kundi la Tahrik-e Taliban Pakistan kama wenzo wa kusukuma mbele gurudumu la malengo yake ya kieneo.

Ahhmad Mansur Khan, mweledi na mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na hili kwamba: Taliban inadhani kwamba, kwa kutumia kadhia ya wanamgambo wa Tahrik-e Taliban Pakistan itaweza kutekeleza mipango yake. Inaonekana kuwa, Taliban inatumia hilo kama kuifanya serikali ya Pakistan ipunguze mashinikizo yake dhidi ya Kabul.

Pamoja na hayo lililo la msingi  na muhimu na tawala na serikali zilizoko madarakani kukubali kubeba dhima na majukumu ya kiujirani. Licha ya kuwa, utawala wa serikali ya Taliban hadi sasa haujatambuliwa kimataifa bali hata na majirani zake, lakini kivitendo Taliban imeonyesha kuwa, sio tu kwamba, haiko tayari kukubali kubeba majukumu ya kiujirani, bali imekuwa ikiwazushia matatizo majirani zake na katika eneo, utendaji ambao bila shaka unamulikwa na kupigwa darubini na walimwengu katika tathmini na uchunguzi wao kwa utendaji wa wanamgambo hao na bila shaka jibu la walimwengu litakuwa hapana kuhusiana na takwa la kuutambua utawala wa Taliban.

Ripoti mbalimbali zinazotolewa na asasi za kimataifa zinaonyesha kuwa, Afghanistan inabadilika taratibu na kuwa kambi ya makundi ya kigaidi, jambo ambalo linakinzana wazi kabisa na nara za awali za wanamgambo wa Taliban.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, Taliban inadhani kwa kuingia katika mvutano na majirani zake na wakati huohuo kukataa kubeba majukumu mkabala na ahadi za kiutawala itaweza kudumisha utawala wake. Hii ni katika hali ambayo, Taliban ambayo ina tajiriba ya kufeli katika kuitawala Afghanistan, hivi sasa inakabiliwa na onyo kutoka kwa madola ya Ulaya hasa kutokana na utendahji wake kutiliwa shaka. Kwa muktadha huo, ili uhai wa kisiasa wa Taliban ubakie, bila shaka wanamgambo hao wanahitaji kushhirikiana na majirani wa Afghanistan na wakati huo huo serikali ya Taliban ikubali kubeba dhima ya majukumu mkabala na majirani zake.

Alaa kulli haal, matamshi ya Bilawal Bhutto Zadrari, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Pakistan ya kuonyesha wasiwasi wa mataifa jirani na Afghanistan ikiwemo Pakistan kuhusiana na kuundwa serikali jumuishi, kuheshimiwa haki za wanawake na mabinti na Afghanistan kutokuwa tishio kwa mataifa jirani ni mambo muhimu ambayo yanafuatiliwa kwa umaanani na duru za kieneo na kimataifa na hatua ya Taliban ya kupuuzwa hayo, kimsingi ni kutangaza makabiliano na jamii ya kimataifa.

Katika hali hii, majirani wa Afghanistan ikiwemo Pakistan wanataraji kuiona serikali ya Taliban ikitekeleza ahadi zake kuhusiana na masuala ya kiusalama na kimaisha na hivyo kuzuia kuibuka mgogoro katika eneo ambapo kwa mujibu wa tangazo la jeshi la Pakistan ni kwamba, mataifa ya eneo likiwemo jeshi la Pakistan lina uwezo na nguvu za lazima za kukandamiza aina yoyote ile ya ukosefu wa usalama na hivyo Taliban haipaswi kuruhusu subira ya mataifa ya eneo ifikie kikomo.