Jun 01, 2023 01:22 UTC
  • Onyo kuhusu kudorora Ulaya katika mfumo unaotawaliwa na Marekani

Mwanafikra mashuhuri wa Marekani Noam Chomsky ameonya kwamba huenda Ulaya ikadhoofika sana kiviwanda ikiwa itaendelea kuwa chini ya utawala wa Marekani.

Katika mahojiano yaliyochapishwa Jumatano, Chomsky amesema: "Ulaya inapaswa kuchukua uamuzi mkubwa iwapo je, itasalia katika mfumo unaotawaliwa na Marekani na pengine ikabiliwe na kuzorota na hata, kulingana na baadhi ya utabiri, kuondolewa hadhi yake ya nguvu ya viwanda; au kwa namna fulani itashirikiana na mshirika wake wa kiuchumi wa asili Mashariki (yaani Russia), ambayo ina rasilimali zote za madini zinazohitajika na Ulaya na ni lango la soko lenye faida kubwa la China"

Onyo la mwanafikra huyo mashuhuri wa Marekani kuhusu matokeo ya Ulaya kutawaliwa na Marekani limetolewa kuhusiana na mielekeo ya sasa katika uwanja wa mahusiano baina ya pande mbili za Atlantiki. Baada ya rais mpya wa Marekani Joe Biden kuchukua madaraka mwishoni mwa Januari 2021, alifanya juhudi kubwa kufufua muungano wa pande mbili za Bahari ya Atlantiki uliozorota wakati wa utawala wa Trump. Lengo lake kuu lilikuwa kutumia tena Ulaya kama chombo cha kutekeleza sera zake za kimataifa. Muungano huo umejidhihirisha zaidi katika baadhi ya nyuga za kisiasa na kiusalama, kama vile msimamo wa Marekani na Umoja wa Ulaya kuhusu kuisiadia Ukriane katika vita na Russia sambamba na kuiwekea Moscow vikwazo. Hali kadhalika pande mbili zimekuwa zikishirikiana kuhusiana na mpango wa mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya Iran maarufu kama  JCPOA ambapo madola hayo ya Maghariebi yanaiwekea vikwazo Iran kutokana na mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani.

Chomsky anasema kuhusu kadhia hii kwamba: Uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine ni jambo ambalo liliibua fursa kubwa kwa Marekani ya kuvuta bara Ulaya katika kambi yake ili kuunda mfumo wenye kuchukua maamuzi ya upande mmoja.

Wakati huo huo, licha ya uhusiano huo baina ya pande mbili za Atlantiki yaani Ulaya na Marekani, Washington imekuwa mshindani mkubwa wa Ulaya kwa kuidhinisha na kufuata mipango kama vile Sheria ya Kupunguza Mfumuko wa Bei (IRA) na kwa hakika inatekeleza jukumu la kudhoofisha uchumi wa Ulaya. Ijapokuwa White House inataja sheria ya IRA kama jaribio la ubunifu la kufufua uzalishaji wa Marekani na kukuza teknolojia mbadala, nchi za Umoja wa Ulaya zinaamini kuwa Marekani imeanzisha vita vya kibiashara na Ulaya kwa kutoa ruzuku yake katika sekta ya uchumi wa kijani. Wakati huo huo, kwa kutoza ushuru kwa bidhaa za makampuni ya Ulaya, itayanyima mashirika hayo fursa ya kushindana na mashirika ya Marekani. Hii inaonyesha kuwa Washington, licha ya kauli mbiu zake, haijatilia maanani maslahi ya washirika wake na inawatumia tu kama chombo cha kufikia malengo yake.

Noam Chomsky

Mtazamo huu unawakilisha muelekeo halisi wa sera za Marekani kuhusu washirika wake barani Ulaya na sehemu zingine za ulimwengu na kimsingi ni mwendelezo wa msimamo wa kujitakia makuu wa kauli mbiu maarufu ya Trump ya "Marekani Kwanza".

Sera na hatua za Marekani wakati wa uongozi wa Joe Biden, ambazo zimeegemezwa kuitumia Ulaya kama chombo cha kudhamini maslahi yake na kudhoofisha nguvu na maslahi ya bara hilo kwa muda mrefu. Sera hizo za Biden zimeibua malalamiko ya baadhi ya viongozi wa Ulaya. Kuhusiana na hilo, Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orbán amesisitiza kuwa sera za serikali ya Joe Biden zimekuwa sababu kuu ya kudorora Ulaya wakati huu wa vita vya Ukraine.

Mchambuzi wa kisiasa Elijah Magnier anasema: Washington inachochea ongezeko la tofauti kati ya madola makuu mawili yenye nguvu katika Umoja wa Ulaya yaani Ujerumani na Ufaransa na imewekeza kiuhakika katika suala la kuibua Ulaya iliyo dhaifu.

Kutokana na ufahamu wa malengo ya Marekani ya muda mrefu, Russia imezionya mara kwa mara nchi za Ulaya kuhusu kuitegemea na kuifuata kibubusa Washington. Katika onyo la hivi punde kuhusiana na hilo, mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa, Vasily Nebenzya amesisitiza katika hotuba yake kwamba mwaka mmoja baada ya Umoja wa Ulaya kukata kabisa uhusiano wake na Russia, ukuaji wake wa uchumi umeshuka hadi karibu sifuri, na wakati huo huo, kuna kiwango cha mfumuko wa bei cha tarakimu mbili ambacho hakijawahi kutokea tena katika nchi za umoja huo.

Tags