China yaitaka Marekani iache undumakuwili, ulaghai wa kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i98614-china_yaitaka_marekani_iache_undumakuwili_ulaghai_wa_kisiasa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema mtazamo na misimamo ya Marekani mkabala wa mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mfano mwingine wa sera za kindumakuwili za Washington.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 10, 2023 06:53 UTC
  • China yaitaka Marekani iache undumakuwili, ulaghai wa kisiasa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema mtazamo na misimamo ya Marekani mkabala wa mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mfano mwingine wa sera za kindumakuwili za Washington.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Wang Wenbin, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China akisema kuwa, Marekani inapasa kuachana na sera zake za kindumakuwili na utapeli wa kisiasa.

Amesema, katika hali ambayo Marekani na Uingereza zinaizuia Iran kurutubisha urani kwa kiwango cha juu, lakini nchi hizo za Magharibi zinapanga kuitumia Australia matani ya madini hayo yaliyorutubishwa kwa zaidi ya asilimia 90.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa China amebainisha kuwa, hatua ya US na UK kuitumia Australia urani kama sehemu ya ushirikiano wa pande tatu wa nyambizi za nyuklia, inaashiria unafiki wa nchi hizo na ukiukaji wa wazi Mkataba wa Kuzuia Uundaji na Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT).

Kituo cha kurutubisha urani cha Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema, "Tunaziomba Marekani, Uingereza na Australia kufungamana na wajibu wao wa kimataifa wa kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia, na kuachana na undumakuwili na ulaghai wa kisiasa."

Wenbin ameongeza kuwa, anatumai Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) utatekelezaji majukumu yake ipasavyuo, ya kupambana na kuzuia uundaji na uenezaji silaha za nyuklia duniani.

Marekani inaishinikiza Iran katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ni mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia NPT, huku ikipuuza miito ya jamii ya kimataifa ya kutaka Israel ilazimishwe kujiunga na mkataba huo.