Kanisa la Anglikana 'lasikitishwa' na sheria dhidi ya ushoga Uganda
Kiongozi wa Kanisa la Kianglikana Duniani amedai kuwa amesikitishwa na hatua ya Uganda ya kupasisha sheria kali ya kupambana na ubaradhuli na mahusiano ya watu jinsia moja.
Justin Welby, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana lenye makao makuu yake mjini Canterbury nchini Uingereza amesema hayo katika taarifa ya jana Ijumaa na kuongeza kuwa, ametiwa kiwewe na simanzi kwa kupitishwa sheria hiyo.
Welby amesema, "Nimemuandikia barua ndugu yangu katika Kristo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini Uganda, Stephen Kaziimba, ili kumbainishia masikitiko yangu na kuchukizwa kwangu na hatua ya Kanisa hilo kuunga mkono Sheria dhidi ya Ushoga."
Kiongozi huyo wa Kanisa la Anglikana Duniani ameongeza kuwa, "Nimemkumbusha Askofu Kiziimba kwamba, Waangalikana kote duniani wamekuwa wakipinga suala la kujinaishwa vitendo vya ushoga, usagaji na watu kubadili jinsia zao (LGBT)."
Februari mwaka huu, viongozi wa Kanisa la Kianglikana barani Afrika walitishia kujitenga na Kanisa mama la Uingereza kwa kubariki na kuruhusu ndoa na mahusiano ya watu wenye jinsia moja.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini Uganda, Stephen Samuel Kaziimba Mugalu alisema: Sisi kama Kanisa la Uganda hatuwezi kuunga mkono ufuska huo, kwani Mungu hawezi kubariki kitu ambacho amekitaja kuwa ni dhambi.
Aidha Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amekataa wito wa nchi za Magharibi wa kufuta sheria hiyo dhidi ya ushoga iliyopasishwa na Bunge la nchi hiyo na kuidhinishwa na yeye mwenyewe mwishoni mwa mwezi uliopita.