Zakharova: Russia itatumia silaha za nyuklia ikilazimu
(last modified Fri, 16 Jun 2023 07:38:05 GMT )
Jun 16, 2023 07:38 UTC
  • Zakharova: Russia itatumia silaha za nyuklia ikilazimu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema nchi hiyo inaweza tu kutumia silaha zake za nyuklia katika mazingira maalum ya kujihami.

Maria Zakharova alisema hayo jana Alkhamisi katika kikao na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, Russia haitatishia nchi yoyote kwa silaha za nyuklia na itatumia tu silaha hizo kulinda usalama wake na kutetea mamlaka yake ya kujitawala.

Ameeleza bayana kuwa, "Hakutakuwa na mshindi iwapo vita vya nyuklia vitaibuka. Daima tumeziasa pande nyingine kwenye mkataba wa nchi tano zenye silaha za nyuklia kuhakikisha vita vya silaha hizo havitokei."

Zakharova amewahi kuonya huko nyuma pia kwamba, sera za kihasama za Marekani kuhusiana na kadhia ya Ukraine zinaweza kufuta makubaliano ya mwisho yaliyosalia ya nyuklia baina yake na Russia.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema nchi za Magharibi zinashindana kutuma silaha Ukraine kwa shabaha ya kuchelewesha oparesheni amilifu ya jeshi la Russia nchini Ukraine.

Nyambizi ya nyuklia ya Russia

Aidha amezishutumu nchi za Magharibi kwa kuchochea moto wa vita vya zaidi ya mwaka mmoja nchini Ukraine ambavyo vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu.

Tayari Rais Vladimir Putin wa Russia ametangaza kwamba, katika kukabiliana na kushadidi kwa shughuli za kijeshi za nchi za Magharibi na ongezeko la msaada wao kwa jeshi la Ukraine, Moscow sasa itapeleka baadhi ya silaha zake za nyuklia za kimbinu huko Belarus. Kwa mujibu Putin, ujenzi wa maghala ya silaha za nyuklia za masafa mafupi nchini Belarus utakamilika ifikapo Julai Mosi.