Mtoto wa miaka 2 ampiga risasi mamake mjamzito Marekani
Mama mjamzito ameaga dunia nchini Marekani baada ya kupigwa risasi na mtoto wake wa miaka miwili katika jimbo la Ohio.
Afisa wa polisi, David Smith ameiambia kanali ya News 5 Cleveland kuwa, mwanamke huyo kwa jina Laura Ilg aliyekuwa na umri wa miaka 31 aliaga dunia akitibiwa hospitalini, baada ya kupigwa risasi mgongoni 'kwa bahati mbaya' na mwanawe wa kiume.
Aidha juhudi za madaktari za kumuokoa mtoto aliyekuwa tumboni mwa mama huyo hazikufua dafu. Tukio hilo la Juni 16 ni katika msururu wa vifo vinavyotokana na umiliki holela wa silaha za moto nchini humo.
Machi mwaka huu, mtoto wa kike wa miaka mitatu alimuua kwa kumpiga risasi dadake wa miaka minne 'bila kukusudia' huko Houston, katika jimbo la Texas, kusini mwa Marekani.
Aidha mapema mwaka huu, mtoto wa miaka sita huko nchini Marekani alitiwa mbaroni baada ya kumpiga risasi na kumjeruhi vibaya mwalimu wake wakiwa darasani katika mji wa Newport News, jimboni Virginia.
Kadhalika Machi mwaka jana, tukio jingine la kusikitisha lilitokea nchini Marekani baada ya mtoto wa miaka mitatu kumuua mama yake kwa kumpiga risasi katika mji wa Dolton.
Maelfu ya raia wa Marekani huuawa kila mwaka katika matukio ya mashambulizi ya silaha za moto katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. Vitendo vya ukatili wa silaha za moto nchini Marekani vimegeuka kuwa moja ya matatizo makubwa na sugu katika jamii ya Marekani, huku makundi ya haki za raia yakitaka kuwepo sheria za kubana umiliki wa bunduki mikononi mwa raia.
Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, maelfu ya watu wanauawa kwa silaha za moto kote Marekani kila mwaka, ambapo kwa wastani nchi hiyo inanakili vifo 116 kwa siku. Matukio 647 ya ufyatuaji risasi kiholela yalirekodiwa mwaka wa 2022 ambapo watu 44,287 waliuawa.