Kremlin yapinga madai ya Macron kwamba Russia 'inayumbisha' amani Afrika
-
Dmitry Peskov
Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin, imekanusha madai ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kwamba Russia inavuruga utulivu barani Afrika na kuituhumu Moscow kwamba imetuma makundi ya mamluki barani humo.
Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amesema: "Russia inaendeleza uhusiano wa kirafiki, unaojenga na kwa msingi wa kuheshimiana na kujali matatizo ya kila upande".
"Uhusiano wetu na nchi zote za Afrika hauelekezwi - na hauwezi kuelekezwa - dhidi ya nchi tatu," amesema Dmitry Peskov.
Jana Ijumaa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alikosoa kile alichosema ni hatua ya Russia ya kutuma mamluki barani Afrika. Macron aliyasema hayo katika mkutano wa kilele wa New Global Financing Pact mjini Paris. Viongozi wengi wa Afrika - ikiwa ni pamoja na kutoka Chad, Gabon, Nigeria na Afrika Kusini - wanahudhuria mkutano huo unaotaka kurekebisha mfumo wa fedha wa kimataifa.
Macron alidai kuwa: "Russia ni nguvu inayovuruga amani barani Afrika kupitia wanamgambo wa kibinafsi ambao wanaenda kufanya dhuluma na ukatili kwa raia."
Katika miaka ya hivi karibuni Moscow imepata ushawishi katika maeneo ambayo Paris ilikuwa ikiyadhibiti kwa karne nyingi, ikiwa ni pamoja na Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mali. Nguvu na ushawishi wa Ufaransa barani Afrika umepungua kutokana na kushindwa wanajeshi wa nchi hiyo kusitisha ghasia za makundi ya waasi katika nchi hizo. Sera za kikoloni za Ufaransa pia zimechangia kuongezeka chuki dhidi ya nchi hiyo katika makoloni ya zamani ya Ufaransa.