Putin: Wamagharibi walitaka kuona Warusi wakiuana wenyewe kwa wenyewe
https://parstoday.ir/sw/news/world-i99248-putin_wamagharibi_walitaka_kuona_warusi_wakiuana_wenyewe_kwa_wenyewe
Rais Vladimir Putin wa Russia amesema aliagiza vikosi vya nchi hiyo vijiepushe na umwagaji damu wakati wa uasi wa kundi la Wagner mwishoni mwa wiki iliyopita, akisisitiza kuwa Ukraine na Wamagharibi walitaka kuona wananchi wa Russia wakiuana wenyewe kwa wenyewe.
(last modified 2025-10-20T07:03:11+00:00 )
Jun 27, 2023 06:56 UTC
  • Putin: Wamagharibi walitaka kuona Warusi wakiuana wenyewe kwa wenyewe

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema aliagiza vikosi vya nchi hiyo vijiepushe na umwagaji damu wakati wa uasi wa kundi la Wagner mwishoni mwa wiki iliyopita, akisisitiza kuwa Ukraine na Wamagharibi walitaka kuona wananchi wa Russia wakiuana wenyewe kwa wenyewe.

Putin alisema hayo jana Jumatatu katika hotuba yake kwa taifa kupitia televisheni na kuongeza kuwa, "Tangu mwanzoni mwa matukio (ya uasi wa Wagner), kwa amri yangu, hatua zilichukuliwa ili kuzuia umwagaji damu mkubwa."

Rais wa Russia ameeleza bayana kuwa, wakati ulihitajika wa kuwapa fursa ya kujirudi waliokuwa wamefanya makosa, ili wafahamu kuwa uamuzi wao ulipingwa na jamii yote ya Warusi.

Sambamba na kuwapongeza wananchi wa Russia kwa umoja na uzalendo, Rais Putin amebainisha kuwa, uzalendo wa Warusi ulitoa pigo kwa maadui wa Russia, Wanazi mamboleo na Kiev, pamoja na walezi wao wa Magharibi, kwani walitaka kuona wanajeshi wa Russia wanauana wenyewe kwa wenywe.

Wanachama wa Wagner

Putin bila kumtaja kiongozi wa Wagner aliyeongoza uasi huo ameongeza kuwa, uasi huo uliwaunganisha Warusi wote na walikuwa tayari kutekeleza wajibu wao wa kuilinda ardhi yao.

Alasiri ya Jumamosi baada ya kufikiwa mapatano ya kukomesha uasi wa Wagner, kiongozi wa kundi hilo, Yevgeny Prigozhin alisema katika ujumbe wa sauti kwamba: "Tumeamua kuwarudisha wapiganaji kwenye kambi zao ili kuepusha umwagaji damu ya Warusi."

Kadhalika Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitiza kuwa, ahadi ya Ikulu ya Kremlin ya kutowafungulia mashitaka wanachama wa kundi la Wagner itaheshimiwa.