Jumatatu, 14 Aprili, 2025
Leo ni Jumatatu tarehe 15 Shawwal 1446 Hijiria, sawa na tarehe 14 Aprili 2025.
Katika siku kama ya leo miaka 144 ilyopita alizaliwa Abu Tufail A'mir bin Wathilah al Kinani ambaye alikuwa miongoni mwa washairi na mahatibu mashuhuri za zama za awali za Uislamu.
Abu Tufail alikuwa miongoni mwa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na alisuhubiana kwa muda mrefu na Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kushiriki katika Vita vya Siffin, Jamal na Nahrawan pamoja na mtukufu huyo.
Abu Tufail alifaidika sana na elimu na maarifa ya mtukufu huyo. Mashari mengi ya A'mir bin Wathilah yanamsifu Mtume Muhammad (saw).

Siku kama ya leo miaka 1194 iliyopita inayosadifiana na tarehe 15 Mfunguo Mosi Shawwal mwaka 252 Hijria, alifariki dunia Abdul-Adhim al Hassani.
Mtukufu huyu ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW kupitia shajara ya Imam Hassan Al-Mujtaba (AS). Abdul-Adhim al Hassani alikuwa mashuhuri sana kwa karama zake nyingi. Maimamu watukufu walithibitisha ukweli na uchamungu wake na walikuwa wakinukuu hadithi kutoka kwake.
Baada ya kushadidi dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Bani Abbas, Abdul-Adhim al Hassani alilazimika kuhajiri na kuhamia mjini Rey kusini mwa Tehran ya leo. Mtukufu huyo anajulikana pia kama shahidi ambaye aliuawa kwa kupewa sumu.
Haram Tukufu ya Abdul-Adhim Hassani ipo katika mji wa Rey na wapezi wa Ahlul Bayt AS kutoka kona mbalimbali za dunia humiminika katika eneo hilo kwa ajili ya kwenda kufanya ziara.

Leo tarehe 25 Farvardin kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi arif na malenga mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani Fariduddin Attar Naishaburi.
Attar Naishaburi alizaliwa karibu mwaka 540 Hijria na baada ya kufariki dunia baba yake ambaye alikuwa muuza madawa, aliendeleza kazi hiyo ya baba na kupata maarifa mengi kuhusu elimu ya tiba. Katika kipindi hicho alipatwa na mabadiliko makubwa na kuanza safari ya ndani ya nafasfi na kutakasa roho.
Alifanya safari katika maeneo mengi ya ulimwengu wa Kiislamu ya kupata elimu ya irfani kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo. Attar Naishaburi ameandika tajiriba na uzoefu wake wa kiirfani katika kalibu ya mashairi na nathari.
Miongoni mwa vitabu vya arifu huyo mkubwa Muirani ni "Tadhkiratul Auliyaa" na "Mantwiqut Twair."

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita aliaga dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Seikh Muhammad Taqi Razi katika mji wa Isfahan nchini Iran.
Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku.
Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid".

Katika siku kama hii ya leo miaka 134 iliyopita muungano wa Pan American ambao baadaye ulibadili jina na kujulikana kama Jumuiya ya Nchi za Amerika uliasisiwa.
Nchi wanachama wa jumuiya hiyo zilikuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali hadi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Hata hivyo baada ya vita hivyo kumalizika Jumuiya ya Nchi za Amerika iliundwa kutokana na kuweko haja ya kupanuliwa zaidi mashirikiano kati ya nchi hizo. Pamoja na hayo yote kitu kinachoitia wasiwasi jumuiya hiyo ni satwa na ushawishi mkubwa wa Marekani katika jumuiya hiyo na hatua yake ya kukitumia vibaya chombo hicho kwa maslahi yake ya kisiasa.
Kwa sababu hiyo nchi wanachama zinafanya jitihada kubwa za kupunguza ushawishi wa Marekani katika jumuiya hiyo.

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, serikali ya Umoja wa Kisovieti ilitia saini makubaliano mjini Geneva na kukubali kuondoa majeshi yake katika ardhi ya Afghanistan.
Jeshi la Umoja wa Sovieti liliiteka na kuikalia kwa mabavu Afghanistan mwaka 1979. Hata hivyo tangu awali majeshi hayo yalikabiliwa na upinzani mkali wa mujahidina wa Kiafghani. Vilevile Marekani nayo iliyokuwa ikiona maslahi yake yamo hatarini nchini Afghanistan, ilitumia wenzo wa kijeshi, kisiasa na kiuchumi dhidi ya Moscow ili kuilazimisha iondoke nchini Afghanistan.

Tarehe 25 Farvardin miaka 36 iliyopita serikali ya wakati huo ya Iraq ilikiri kwamba ilitumia silaha za kemikali katika vita vyake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika kipindi chote cha miaka minane ya vita hivyo Iran iliwasilisha mashtaka katika jumuiya za kimataifa kwamba Iraq inatumia silaha za kemikali dhidi ya wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu.
Wakati huo Iraq haikukiri wala kukadhibisha habari hiyo. Hata hivyo katika siku kama hii ya leo wakati vita vilipokuwa vimepamba moto, serikali ya Baghdad ilikiri kwamba inatumia silaha za kemikali zikiwemo za gesi ya sumu na hatari ya haradali dhidi ya maeneo ya kijeshi na kiraia ya Iran.
Takwimu zimeonesha kwamba utawala wa Baath wa Iraq ulifanya mashambulizi 3,500 kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote cha vita hivyo.

Miaka 22 iliyopita katika siku kama leo, Hugo Chavez rais wa zamani wa Venezuela alirejea nchini kwake na kushika hatamu za uongozi baada ya kufeli jaribio la mapinduzi ya kumuondoa madarakani. Chavez Aliingia madarakani mwaka 1999 na kufanya mabadiliko makubwa kwa maslahi ya tabaka la chini.
Vilevile alichukua hatua za kusimamia mashirika ya mafuta ya Kimarekani yaliyokuwa yakichimba mafuta ya nchi hiyo. Siasa za kujitegemea za Chavez ziliikasirisha sana Washington. Ni kwa sababu hiyo, ndiyo maana Marekani ilipanga na kuratibu mapinduzi mnamo tarehe 12 Machi mwaka 2002. Licha ya mapinduzi hayo kupata mafanikio katika hatua za awali, lakini wananchi wa Venezuela waliokuwa wameridhishwa na mabadiliko ya Chavez, walipinga uingiliaji wa nchi za nje katika masuala ya ndani ya nchi yao.
Hugo Chavez alifariki dunia Machi 5 mwaka 2013 kutokana na maradhi ya saratani akiwa na umri wa miaka 58.
