Jumatatu, 26 Januari, 2026
https://parstoday.ir/sw/radio/event-i135892-jumatatu_26_januari_2026
Leo ni Jumatatu 6 Sha'ban 1447 Hijria ambayo inasadifiana na 26 Januari 2026.
(last modified 2026-01-26T02:36:13+00:00 )
Jan 26, 2026 02:36 UTC
  • Jumatatu, 26 Januari, 2026

Leo ni Jumatatu 6 Sha'ban 1447 Hijria ambayo inasadifiana na 26 Januari 2026.

Miaka 203 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Edward Jenner tabibu wa Kiingereza aliyegundua chanjo ya ndui yaani (small pox).

Jenner alizaliwa mwaka 1749. Tabibu huyo alifanikiwa kugundua chanjo ya ndui akiwa na umri wa miaka 45 wakati alipoelekea nchini India.

Kuanzia hapo ugonjwa huo wa ndui ulitibiwa kwa kutumia chanjo hiyo. mwaka 1979 maradhi hayo yalitokomezwa kabisa duniani. *** 

Miaka 122 iliyopita katika siku kama ya tarehe, 6 Sha'ban 1325 Hijria aliuawa shahidi Allama Ibrahim Khui alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu.

Alifanikiwa kupata daraja ya Ijihadi baada ya kusoma kwa miaka mingi kwa walimu mahiri wa zama hizo kama Sheikh Murtadha Ansari. Allama Ibrahim Khui alikuwa na umahiri wa aina yake katika elimu mbalimbali hususan falsafa.

mwanazuoni huyo wa Kiirani alifanya na harakati na juhudi kubwa katika zama za kupigania utawala wa katiba, kupinga dhulma na kupigania uhuru. Hatimaye katika siku kama ya leo aliuawa shahidi akiwa nyumbani kwake na makachero wa Muhammad Ali Shah, mmoja wa watawala madikteta wa ukoo wa Qajar. ***

Miaka 97 iliyopita katika siku kama ya leo, Mirza Lutf-Ali Nasiri alimu, mwanafasihi na mahiri na mtajika wa Kiirani aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 82.

Alitambulika kwa lakabu ya Sadru-Afaadhil na alikuwa msomi na mwanazuoni mashuhuri katika karne ya 14. Lutf-Ali Nasiri akiwa pamoja na baba yake na wakati huo akiwa mtoto mdogo alihajiri kutoka Shiraz na kuja katika mji wa Tehran.

Awali alisoma misingi ya hati na baadaye akaichagua fani ya fasihi. Baadaye aliingia katika uwanja wa masomo kama ya usul, fiqhi, Hadithi, tafsiri ya Qur'ani, mantiki na hisabati. ***

Katika siku kama ya leo miaka 76 iliyopita mfumo wa Jamhuri ulitangazwa nchini India na siku hii ikapewa jina la Siku ya Kitaifa ya India.

Baada ya India kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza Jawaharlal Nehru alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu huku Rajendra Prasad akichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mfumo wa India, wadhifa wa urais ni wa kiheshima tu na Waziri Mkuu ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za serikali. India ina jamii ya karibu watu bilioni moja na nusu na ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa zaidi duniani baada ya China. ***

Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya Kiislamu wa Ujerumani, Bi Annemarie Schimmel.

Bibi Schimmel alipendelea mno kutalii na kupata maarifa kuhusu ustaarabu wa Kiislamu na alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya masuala ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Berlin akiwa na umri wa miaka 19. Prf. Annemarie Schimmel alifundisha kwa miaka mingi historia ya dini na irfani ya Kiislamu katika vyuo vikuu vya Marekani, Ujerumani na Uturuki.

Mbali na kujua lugha za Kijerumani na Kiingereza, Bi Schimmel alijifunza pia lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kiurdu, Kibengali na Kituruki kwa ajili ya kupata maarifa zaidi kuhusu masuala ya Kiislamu. 

Prf. Annemmarie Schimmel ameandika vitabu kadhaa kuhusu masuala ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kile cha "Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu" na "Mwanamke katika Irfani ya Kiislamu".   ****