Jumatano, 04 Februari, 2026
https://parstoday.ir/sw/radio/event-i136222-jumatano_04_februari_2026
Leo ni Jumatano tarehe 15 Sha'ban 1447 Hijria sawa na 04 Februari 2026.
(last modified 2026-02-10T07:17:34+00:00 )
Feb 04, 2026 02:18 UTC
  • Jumatano, 04 Februari, 2026

Leo ni Jumatano tarehe 15 Sha'ban 1447 Hijria sawa na 04 Februari 2026.

Siku kama ya leo miaka 1192 iliyopita alizaliwa Imam Mahdi AS mwokozi wa ulimwengu katika mji wa Samarra, kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq.

Yeye ni mwana mpendwa wa Imam Hassan Askari AS ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW. Miongoni mwa lakabu mashuhuri za Imam huyo wa Zama ni Mahdi, ambayo ina maana ya mtu aliyepewa hidaya na kuongozwa, na al Qaim, kwa maana ya atakayeanzisha mapambano.

Imam Mahdi AS alipitisha miaka mitano ya kwanza ya uhai wake akiwa chini ya malezi ya baba yake mpendwa, Imam Askari AS. Alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu kama Imam baada ya kuuawa shahidi baba yake mtukufu na kisha akatoweka na kwenda ghaiba kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu.

Kwa muda wa miaka 69 mtukufu huyo alikuwa akiwasiliana na kuwaongoza Waislamu kupitia wawakilishi wake maalumu. Baada ya hapo na kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Imam Mahdi AS alienda kwenye ghaiba kubwa na ya muda mrefu na atadhihiri tena ulimwenguni wakati mwafaka ambao Mwenyezi Mungu ataona unafaa.

Atakapodhihiri duniani, ataijaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa baada ya kujaa dhulma na uonevu. Siku ya kuzaliwa mtukufu huyo huadhimishwa nchini Iran kama Siku ya Waliodhulumiwa Duniani. 

Tunatoa mkono wa kheri na baraka kwa wapenda haki wote na hasa wafuasi wa kweli wa Ahlul Bayti wa Bwana Mtume Muhammad SAW kwa mnasaba wa kuchomoza nuru hiyo ya haki.    ******

Siku kama hii ya leo miaka 338 iliyopita Pierre Marivaux mwandishi wa riwaya na michezo ya kuigiza wa Kifaransa alizaliwa huko Paris nchini Ufaransa.

Pierre alianza kujishughulisha na kazi ya sanaa tangu akiwa kijana na kwa muda fulani alishiriki pia katika michezo ya kuigiza hadi pale alipoanza kuandika michezo hiyo.

Marivaux alipata umashuhuri mkubwa kutokana na ukosoaji wake katika uandishi wa riwaya. Marivaux ameacha athari nyingi za kimaandishi zikiwemo riwaya na michezo ya kuigiza ambapo miongoni mwake tunaweza kuashiria zile alizozipa majina kama ya The Prudent na Equitable Father, The Triumph of Love na The Life of Marianne.    *****

Katika siku kama ya leo miaka 81 iliyopita kulifanyika mkutano uliojulikana kwa jina la Yalta katika peninsula ya Crimea huko kusini mwa Urusi ya zamani.

Mkutano huo uliwakutanisha pamoja  viongozi wa nchi za Uingereza, Marekani na Shirikisho la Urusi ya zamani (Churchill, Roosevelt na Stalin). Mkutano huo ulifanyika baada ya kudhihiri dalili za kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia.

Lengo hasa la mkutano wa Yalta lilikuwa kujadili hali ya kisiasa na kijeshi ya nchi zilizokuwa zikipigana vita hivyo, ikiwa ni pamoja na kuainisha hatima ya ardhi zilizokuwa chini ya madola waitifaki.    *****

Miaka 78 iliyopita katika siku kama ya leo nchi ya Sri Lanka ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza.

Nchi hiyo iliyoko kusini mashariki mwa India ilivamiwa na wakoloni wa Kireno katikati mwa karne ya 16 na baadaye wakoloni wa Kiholanzi na tangu mwaka 1798 iliunganishwa rasmi na makoloni ya Uingereza. Mapambano ya kupigania uhuru wa Sri Lanka yalianza mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Mwaka 1931 Uingereza ililazimika kutoa haki ya kutoa maoni kwa wananchi wa Sri Lanka na kuasisi baraza la kutunga sheria na baraza la utekelezaji. Hata hivyo nchi hiyo ilikuwa bado haijapata uhuru kamili katika masuala ya kigeni. Kwa msingi huo mapambano ya wananchi yaliendelezwa hadi kisiwa hicho kilipopata uhuru kamili mwaka 1948.     *****

Katika siku kama ya leo miaka 47 iliyopita wakati mapambano ya wananchi dhidi ya utawala wa Shah yalipokuwa yamefika kileleni, Waziri Mkuu wa utawala wa kifalme hapa nchini Shapour Bakhtiar alifanya jitihada za kuzima vuguvugu la wananchi bila ya mafanikio yoyote. Bakhtiar alisema katika mahojiano na vyombo vya habari kwamba, hatamruhusu Imam Khomeini kuunda serikali ya mpito. Wakati huo uasi wa kiraia, kukimbia wanajeshi na kujiunga na safu za wananchi katika miji mbalimbali ya Iran ikiwa ni pamoja na kujiuzulu wabunge, viongozi wa ngazi za juu serikali na kadhalika viliifanya serikali ipoteze udhibiti wa mambo ndani ya nchi. ***

Na siku kama ya leo miaka 10 iliyopita aliaga dunia Raghib Mustafa Ghalwash qarii na msomaji Qur'ani mahiri wa Kimisri.

Ghalwash alizaliwa Julai 5 mwaka 1938 nchini Misri na kukulia katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na Qur'ani. Raghib Mustafa Ghalwash alikuwa tayari amehifadhi Qur'ani nzima katika rika la ubarobaro na kuanza kusoma kitabu hicho katika hafali na majlisi mbalimbali akiwa na umri wa miaka 16.

Sheikh Raghib Mustafa Ghalwash alikuwa miongoni mwa wasomaji wa Qur'ani waliofanya safari nchini Iran baada ya kumalizika vita vya kulazimishwa vilivyoanzisha na Iraq dhidi ya Iran.

Qiraa na kisomo cha gwiji huyo wa Misri kilipendwa sana nchini Iran. Hatimaye Qarii huyo mashuhuri aliaga dunia alfajiri ya Alkhamisi tarehe 4 Februari mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 77 baada ya kuugua kwa muda mrefu.