Sep 04, 2023 10:50 UTC
  • Sura ya Annajm, aya ya 1-18 (Darsa ya 965)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 965. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 52 ya At-T'uur, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya sura ya 53 ya Annajm. Sura hii iliteremshwa Makka na inaanza kwa kubainisha utaratibu wa kuteremshwa Wahyi kwa Bwana Mtume Muhammad SAW na safari ya Miiraji ya mtukufu huyo. Suratu-Nnajm, ambayo ina aya 62, inakanusha pia khurafa na mambo ya uzushi ya washirikina na kutilia mkazo adhabu za duniani na akhera zitakazowafika watu hao. Baada ya utangulizi huo mfupi, sasa tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya mwanzo hadi ya nne ya sura hiyo ambazo zinasema:

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa Jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

وَالنَّجْمِ إِذَا هَوَىٰ

Naapa kwa nyota inapo tua,

مَا ضَلَّ صَاحِبُكُمْ وَمَا غَوَىٰ

Mwenzenu (huyu) hakupotea, wala hakukosea.

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ

Wala hatamki kwa matamanio.

إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa;

Kama zilivyo baadhi ya sura za Makka, Suratu-Nnajm, nayo pia imeanza kwa kiapo; kiapo cha kuapiwa nyota, ambayo ni moja ya vitu vya kimaumbile, ambacho kimekuwa kikipewa umuhimu mkubwa na wanadamu katika zama zote za historia mpaka ikafika hadi katika baadhi ya vipindi vya historia, nyota zikawa ni kitu kinachoabudiwa na baadhi ya kaumu za watu. Baada ya kiapo hicho, Allah SWT anawahutubu wakazi wa Makka kwa kuwaambia: Muhammad Ibn Abdillah, ambaye amezaliwa katika jamii yenu, amekuwa akiishi na kuchanganyika na nyinyi kwa zaidi ya miaka 40. Kwa muda wote huo, nyinyi hamjawahi kusikia neno lolote baya kutoka kinywani mwake wala tabia yoyote mbaya katika matendo yake, bali nyote mnashuhudia kuwa yeye ni mkweli na mwaminifu kwenu. Kwa hivyo kama leo amekujieni na kukwambieni kwamba ametumwa na Mwenyezi Mungu kukuleteeni uongofu, hafanyi hivyo kwa matamanio ya nafsi yake wala kwa kupenda jaha na ukubwa, mkadhani kwamba anataka akutawalini na kuwa juu yenu au anapigania mali na hadhi yoyote katika jamii yenu. Anayokulinganieni ni maneno ya Mwenyezi Mungu anayomteremshia yeye kwa njia ya Wahyi; basi mwaminini na mufuate anayokuambieni. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kwa kawaida, Mitume huwa wanakulia kwenye kaumu na makabila ya watu waliopotoka na kupotea katika kufuata njia ya haki, lakini wao wenyewe hawakuwahi katu kuathiriwa na fikra, imani, mila na desturi mbovu za jamii zao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, watu ambao hawako tayari kuikubali haki, hujaribu kutafuta kisingizio cha kuikwepa na kuipa mgongo kwa kuwatuhumu waja wema na wateule wa Allah kuwa eti wana uchu wa vyeo na jaha. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, maneno ya Mtume hayatokani na matashi ya nafsi yake wala hayaathiriwi na mazingira ya jamii anayoishi. Vilevile aya hizi zinatutaka tujue kuwa, maneno ya Mtume ni hoja ya kisharia; awe anayasema moja kwa moja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, au ayaamuru yatekelezwe kupitia kauli yake yeye mwenyewe.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya tano hadi ya 12 ya sura yetu ya An Najm, ambazo zinasema:

عَلَّمَهُ شَدِيدُ الْقُوَىٰ

Amemfundisha Mwenye nguvu sana, 

ذُو مِرَّةٍ فَاسْتَوَىٰ

Mwenye kutua, akatulia,

وَهُوَ بِالْأُفُقِ الْأَعْلَىٰ

Naye yuko juu kabisa upeo wa macho.

 ثُمَّ دَنَا فَتَدَلَّىٰ

Kisha akakaribia na kukaribia zaidi. 

فَكَانَ قَابَ قَوْسَيْنِ أَوْ أَدْنَىٰ

Akawa umbali wa pinde mbili, au karibu zaidi.

فَأَوْحَىٰ إِلَىٰ عَبْدِهِ مَا أَوْحَىٰ

Akamfunulia mja wake (Mwenyezi Mungu) alicho mfunulia.

 مَا كَذَبَ الْفُؤَادُ مَا رَأَىٰ

Moyo haukusema uwongo uliyo yaona.

 أَفَتُمَارُونَهُ عَلَىٰ مَا يَرَىٰ

Je! Mnabishana naye kwa aliyo yaona?

Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia asili ya kuteremshwa Wahyi, aya hizi tulizosoma zinaashiria namna Bwana Mtume SAW alivyokuwa akiwasiliana na Allah SWT na kueleza kwamba: Mwalimu wa Mtume ni Mwenyezi Mungu Aliye Mjuzi na Mwenye Hikima ambaye mamlaka yote ya ulimwengu yako mikononi mwake na ayafanyayo Yeye Mola ni imara na thabiti. Alivyo Yeye Mola ni kwa namna isiyoweza kutasawirika katika fikra na akili ya mwanadamu; na hakuna mtu yeyote awezaye kumfikia na kumdiriki Yeye; lakini Mtume wake mteule na mbora wa viumbe wake, Muhammad SAW, aliweza kumshuhudia kwa njia ya batini kupitia nafsi na moyo wake uliokamilika kiimani; ushuhudiaji ambao hauwi na nakisi au upungufu wowote na ndio uliomwezesha Bwana Mtume SAW kuwa karibu na Allah kwa kiwango cha juu kabisa kinachowezekana kumkurubia kiroho Yeye Mola. Ukaribiaji huo ndio ulioandaa mazingira ya kueteremshwa Wahyi; na baada ya hapo, Jibril, -akiwa ndiye wasita na kiunganishi kati ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake-, akawa anamfikishia Wahyi Bwana Mtume, na yeye Mtume SAW akawa anawasomea watu aya hizo za Qur'ani tukufu. Wakanushaji wa Utume katika zama zote za historia walikuwa kila mara wakiona ni jambo lisilowezekana kuwepo mawasiliano kati ya Mwenyezi Mungu na mwanadamu na kwa hivyo wakiukataa ukweli huo. Ilhali mawasiliano hayo, si ya kutumia hisi na hali za kimwili, bali ni mawasiliano ya ushuhudiaji wa moyo na nafsi na ndio maana aya hizi pia zinasisitiza na kueleza bayana kuwa, Bwana Mtume SAW alimuona Mwenyezi Mungu kwa moyo wake, yaani kwa ushuhudiaji wa kiroho, si kwa macho haya mawili tuyajuayo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, si elimu za jarabati na zilizobuniwa na wanadamu, ndizo pekee zinazohitajia mwalimu na mfundishaji. Ili kupevuka na kufikia ukamilifu wa kiroho na kimaanawi, mwanadamu anahitaji pia mwalimu wa mafunzo ya mbinguni ambaye ni Allah SWT, na kuhakikisha anawafundisha watu yale aliyofunzwa yeye na Mola ili kuwaokoa na hatari ya kutumbukia kwenye lindi la khurafa na uzushi na fikra batili na potofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ili kuwajibu watu waliokuwa wakiitakidi kwamba Mtume alikuwa akifunzwa na mwanadamu, aya hizi zinasisitiza na kueleza kinagaubaga kuwa Allah SWT ndiye mwalimu wa Bwana Mtume, na kwamba Wahyi anaowafikishia watu anaupokea kutoka kwenye chimbuko na chemchemi yake kuu, yaani Yeye Mola. Wa aidha aya hizi zinatuonyesha kuwa anapotaka Allah SWT -na kwa idhini yake-, Mtume wake huweza kufikia daraja ya ukuruba, kukawa hakuna tena wasita na kiunganishi baina yake Yeye Mola na mja wake kwa kuweza Mtume kusemezwa na kupokea maneno ya wahyi moja kwa moja. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa, kudhihirisha uja halisi kwa Allah na kujikurubisha kwake Yeye Mola ndiko kunakoandaa mazingira ya kushushiwa Wahyi na kufikia mja cheo na daraja ya kupewa Utume. Na ndio maana aya tulizosoma zinasema: Mwenyezi Mungu alimteremshia Wahyi mja wake na wala hazituambii: Mwenyezi Mungu alimfunulia Wahyi Mtume wake.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 13 hadi 18 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ

Na alimwona mara nyingine,

عِندَ سِدْرَةِ الْمُنتَهَىٰ

Penye Mkunazi wa kumalizikia (mambo yote)

عِندَهَا جَنَّةُ الْمَأْوَىٰ

Karibu yake ndiko kuna hiyo Bustani inayo kaliwa. 

إِذْ يَغْشَى السِّدْرَةَ مَا يَغْشَىٰ

Kilipo ufunika huo Mkunazi hicho kilicho ufunika.

مَا زَاغَ الْبَصَرُ وَمَا طَغَىٰ

Jicho halikuhangaika wala halikuruka mpaka.

لَقَدْ رَأَىٰ مِنْ آيَاتِ رَبِّهِ الْكُبْرَىٰ

Kwa yakini aliona katika Ishara kubwa kabisa za Mola wake Mlezi. 

Aya hizi zinaendelea kuzungumzia kadhia ya Miiraji ya Bwana Mtume SAW, ambayo imezungumziwa pia katika aya ya mwanzo ya Suratul-Israa. Aya zilizotangulia zilielezea namna mtukufu huyo alivyoshuhudia mambo kwa hisi za batini za macho ya moyo; na aya hizi tulizosoma zinasimulia kuhudhuria Mtume mwenyewe mbinguni na kushuhudia kwa macho yake aya, alama na ishara za adhama ya Mwenyezi Mungu katika ulimwengu wa uumbaji. Vilevile zinasimulia jinsi Bwana Mtume Muhammad SAW alivyoiona Pepo ya Allah huko mbinguni, ambako ni mahali zinakokuweko roho za waumini na waja wema na safi hadi kitakaposimama Kiyama, tena chini ya kivuli cha matawi ya mti uliojaa matunda uitwao Sidratul-Muntaha. Katika safari ya Miiraji, Bwana Mtume SAW alijionea kwa macho yake hakika nyingi za mambo, kama ilivyokuwa kwa Nabii Ibrahim AS, ambaye Allah SWT anasema katika aya ya 75 ya Suratul-An’aam kwamba alimuonyesha adhama ya ufalme wake wa mbingu na ardhi, naye akaishuhudia adhamu hiyo. Kwa hivyo tunaweza kusema kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwaonyesha adhama ya uumbaji wake, Mitume wake aliowapa jukumu la kufikisha kwa watu ujumbe na wito wa uongofu. Kufanya hivyo kuliwafikisha Manabii hao kwenye yakini kamili na hivyo kuupokea Wahyi kwa imani na uhakika kamili na kuufikisha kwa watu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mitume wamediriki kumfikia Allah kwa macho ya moyo na wameishuhudia adhama ya uumbaji wa Mola kwa macho haya ya kawaida. Jengine tunalojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa, mbali na Pepo ya Akhera itakayokuwepo baada ya kusimama Kiyama, katika ulimwengu wa barzakhi pia kuna Pepo ambayo waja safi na wema wanastareheshwa ndani yake kwa neema mbalimbali za Allah. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 965 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze imani ya yakini nyoyo zetu, ayape basira ya yakini macho yetu na atupe hatima njema, sisi ni wapendwa wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags