Sep 26, 2023 07:11 UTC
  • Sura ya Al-Qamar, aya ya 1-8 (Darsa ya 969)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 969. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 53 ya An-Najm, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya sura ya 54 ya Al-Qamar. Sura hii iliteremshwa Makka na aya zake zinatoa maonyo na indhari kwa washirikina na wapinzani wa haki. Inabainisha pia hatima za kaumu zilizopita za watu waovu, ambao waliasi wito waliofikishiwa na Mitume wa Mwenyezi Mungu kutokana na inadi na ukaidi wao. Inabainisha hayo ili kuwaasa washirikina waache upinzani wa kumpinga na kumkadhibisha Bwana Mtume Muhammad SAW na badala yake wajisalimishe mbele ya haki. Baada ya utangulizi huo mfupi, sasa tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya mwanzo hadi ya tatu ya sura hiyo ambazo zinasema:

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa Jina la Allah, Mwingi wa Rehma Mwenye Kurehemu

اقْتَرَبَتِ السَّاعَةُ وَانشَقَّ الْقَمَرُ

Kiyama kimekaribia, na mwezi umepasuka!

وَإِن يَرَوْا آيَةً يُعْرِضُوا وَيَقُولُوا سِحْرٌ مُّسْتَمِرٌّ

Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: Huu uchawi tu unaoendelea.

 وَكَذَّبُوا وَاتَّبَعُوا أَهْوَاءَهُمْ ۚ وَكُلُّ أَمْرٍ مُّسْتَقِرٌّ

Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao. Na kila jambo limewekwa kwa wakati wake.

Aya za mwanzo za Suratul-Qamar zinaashiria moja ya miujiza mikubwa ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Ili kupata njia na kisingizio cha kuukadhibisha na kuupinga wito wa Bwana Mtume, washirikina wa Makka walimtaka mtukufu huyo awafanyie jambo ambalo kwa mawazo yao, walidhani kwamba hataweza katu kulifanya. Walimwambia Nabii Muhammad SAW, "kama uyasemayo ni kweli kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, tupasulie mwezi ugawanyike vipande viwili!" Wao walikuwa wakiamini kuwa uchawi na mazingaombwe una taathira katika vitu vya ardhini, lakini hauwezi kuwa na athari katika vitu vya mbinguni; kwa hivyo kama kweli mwezi utapasuka hapo ndipo itapodhihiri kwamba ayafanyayo Muhammad, si uchawi au mazingaombwe. Kufuatia takwa hilo la washirikina, Bwana Mtume SAW alimuelekea Mola wake na kumuomba amtimizie sharti walilompa wapinzani hao wa haki. Kwa idhini ya Allah Jalla Jalaaluh, katika usiku mmoja wakati mwezi ulipokuwa duara kamili, kwa ishara ya Bwana Mtume, ulipasuka katikati na kugawanyika nusu mbili; na baada ya watu wa Makka kulishuhudia tukio hilo kwa macho yao, mwezi ukarudi tena kwenye hali yake ya mwanzo. Lakini pamoja na hayo, wapinzani wa haki ambao hawakutarajia katu kujiri tukio hilo la muujiza, walitia ulimi puani na kudai kwamba huo pia ulikuwa uchawi na mazingaombwe. Walimkadhibisha Bwnaa Mtume SAW kwa kumwambia, "ukweli ni kwamba mwezi haukupasuka na kugawanyika vipande viwili. Ulichofanya wewe, kama wafanyavyo wachawi wengine, ni kutuzuga kwa kiinimacho ili tuhisi na kudhani kuwa mwezi umepasuka na kugawanyika nusu mbili". Lakini kinyume na madai hayo ya washirikina, ukweli ni kwamba, tukio hilo la kupasuka mwezi lilijiri kweli, kiasi kwamba wasafiri wa misafara ya Sham na Yemen walilishuhudia hilo walipokuwa njiani katika safari zao; na hata watu wa ardhi ya Bara Hindi, nao pia walijionea kwa macho yao muujiza huo wa kupasuka mwezi. Qur'ani tukufu inaendelea kueleza kwamba, chimbuko la ukadhibishaji huo ni hawaa na matamanio ya nafsi ambayo humbana mtu asikubali kuifuata haki na badala yake apendelee kila mara kufanya mambo kwa kufuata matamanio na matashi ya nafsi yake. Lakini mwishowe ukweli utadhihirika; na shirki na ukafiri havitakuwa na hatima nyingine isipokuwa kuporomoka na kuangamia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kujiri kwa Kiyama ni hakika isiyo na shaka na kunakaribia; na hili ni onyo na indhari kali kwa walioghafilika nacho na juu ya yale watakayokwenda kuulizwa na kusailiwa kwayo siku hiyo. Kubaathiwa na kupewa Utume Nabii wa Mwisho wa Allah, Muhammad SAW nayo pia ni ishara mojawapo inayoonyesha kuwa mwisho wa dunia unakaribia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mbali na Qur'ani ambayo ni muujiza wa milele wa Bwana Mtume SAW, mtukufu huyo alikuwa na miujiza mingine pia. Kupasuka mwezi na kugawika sehemu mbili sawasawa, ulikuwa moja ya miujiza muhimu zaidi kati ya hiyo. Wa aidha aya hizi zinatuonyesha kwamba, kwa watu walio wakaidi, hata kama watauona muujiza kwa macho yao, wataendelea kupinga kwa kusema huo ni uchawi na mazingaombwe na kumkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa, kufuata matamanio ya nafsi ni moja ya sababu muhimu zaidi zinazowafanya wapinzani wawe wakaidi na wasiwe tayari kuukubali ukweli waliolinganiwa na Mitume.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya nne na ya tano za sura hii ya Al-Qamar ambazo zinasema:

وَلَقَدْ جَاءَهُم مِّنَ الْأَنبَاءِ مَا فِيهِ مُزْدَجَرٌ

Na bila ya shaka zimewajia khabari zenye makaripio.

حِكْمَةٌ بَالِغَةٌ ۖ فَمَا تُغْنِ النُّذُرُ

Hikima kamili; lakini maonyo hayafai kitu! 

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia na kueleza kwamba; kukaidi na kuasi wapinzani wito wa Mtume wa Allah hakufanyiki kwa utovu wa uelewa; kwa sababu wao wanajua ni hatima gani iliwapata watu wa kaumu zilizopita, na vipi waliangamizwa kutokana na kuasi kwao na kwa maovu waliyofanya. Waliwasikia wafuasi wa dini zilizopita wakisema, baada ya kifo kitasimamishwa Kiyama na kwamba huko akhera kuna Pepo na Moto, lakini pamoja na hayo wao washirikina hawataki kuacha maovu na maasi wanayofanya. Lisilo na shaka  ni kuwa anachofanya Allah SWT na Mitume wake ni kutimiza dhima ya kuhakikisha maneno ya haki na hekima yanawafikia watu, ijapokuwa wengi wao hawayajali maonyo na indhari wanazopewa; na kutojali kwao huko hakutawafalia kitu wala kuwa na faida yoyote kwao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kusoma na kutalii historia za waliotangulia kunaweza kumsaidia mtu kufahamu sababu za kuangamizwa kaumu na staarabu zilizopita na kumfanya aache kufru, madhambi na maasi anayofanya. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa jumbe na mafunzo ya Qur'ani yamesimama juu ya msingi wa hekima na mantiki; na yanaweza kufahamika na kukubaliwa na akili za watu wote wa kawaida. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba,  Mitume walitimiza wajibu wao na kukamilisha dhima yao kwa wanadamu wote kwa kuwafikishia wito wa haki; lakini hawawalazimishi wala kuwateza nguvu watu wauamini na kuufuata wito wao. Inatakiwa watu waikubali haki kwa hiari yao wenyewe.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya sita hadi ya nane ya Suratul-Qamar ambazo zinasema:

فَتَوَلَّ عَنْهُمْ ۘ يَوْمَ يَدْعُ الدَّاعِ إِلَىٰ شَيْءٍ نُّكُرٍ

Basi jiepushe nao. Siku atakapo ita mwitaji kuliendea jambo linalotisha;

خُشَّعًا أَبْصَارُهُمْ يَخْرُجُونَ مِنَ الْأَجْدَاثِ كَأَنَّهُمْ جَرَادٌ مُّنتَشِرٌ

Macho yao yatainama; watatoka makaburini kama kwamba wao ni nzige walio tawanyika, 

‏ مُّهْطِعِينَ إِلَى الدَّاعِ ۖ يَقُولُ الْكَافِرُونَ هَٰذَا يَوْمٌ عَسِرٌ

Wanamkimbilia mwitaji, huku makafiri wanasema: Hii ni siku ngumu.

Baada ya aya zilizotangulia kubainisha ubishi na ukaidi wa makafiri na wakanushaji wa haki, aya hizi tulizosoma zinamhutubu Bwana Mtume SAW kwa kumwambia: watu hao waache kama walivyo waendelee na mambo yao na badala yake waendee watu walio tayari kuiamini na kuifuata haki. Watu hao watakuja kuamka na kuzinduka wakati watakapokiona Kiyama kwa macho yao, wakati wafu wote watakapotoka mmoja mmoja ardhini kwa amri ya Mwenyezi Mungu wakielekea huku na kule kwa woga, hofu na mshtuko. Hali na mazingira ya Kiyama yatakuwa kitu kigeni kwa watu hao na watakuwa wanapiga mbio kukimbilia kila inakosikika miito na sauti kwa kutaka kujua kinachoendelea ili wapate utulivu. Lakini kadiri watakavyosonga mbele ndivyo watakavyozidi kutambaliwa na hofu na mshtuko na kubaini kuwa hii ndiyo ile siku waliyokuwa wakielezwa habari zake duniani lakini wakawa wanaikadhibisha. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, baada ya kutimiza dhima na jukumu letu la kuwafikishia wapinzani wito wa haki, wakati mwingine huwa inapasa tuachane nao kwa kuwaacha kama walivyo ili wasije wakadhani kuwa sisi ni wahitaji wa wao kusilimu au kuikubali haki na kwamba tunawaomba na kuwabembeleza waifuate haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mandhari za Siku ya Kiyama zitakuwa ngumu, nzito na za kutisha kwa makafiri na watu waovu, kwa sababu zitakuwa na hali na mazingira ambayo wao hawakutarajia hata kidogo kukabiliana nayo. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, maadi na kufufuliwa kwa viumbe, kutakuwa katika sura na hali ya kimwili; na watu wenyewe watafufuka na kutoka chini ya ardhi; si kwamba zitakazofufuliwa siku hiyo ni roho zao tu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 969 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

 

Tags