Oct 06, 2023 02:48 UTC
  • Ijumaa, tarehe 6 Oktoba, 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 20 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1445 Hijria sawa na Oktoba 6 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 995 iliyopita yaani tareher 20 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka 450 Hijria, alifariki dunia Abu Tayyib Tabari, faqihi na mwandishi wa Kiislamu huko Baghdad. Abu Tayyib alizaliwa mwaka 348 Hijria huko Amol, moja kati ya miji ya kaskazini mwa Iran. Tabari alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa lengo la kutafuta elimu. Abu Tayyib Tabari, aliishi na kufundisha huko Baghdad ambapo alikuwa miongoni mwa maulamaa wakubwa za zama zake. Faqihi Tabari alikuwa hodari katika taaluma ya fasihi na utunzi wa mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu mbalimbali na miongoni mwa vitabu hivyo ni "Jawab fi Sima'a" na "al Ghinaa wa Al Ta'aliqatil Kubra fil Furu'u.

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita sawa na tarehe 6 Oktoba mwaka 1973, vilianza vita vya nne kati ya Waarabu na utawala ghasibu wa Israel. Katika siku hiyo jeshi la Misri lilivishambulia vikosi vya utawala huo haramu katika oparesheni ya kushtukiza katika upande wa pili wa Mfereji wa Suez. Baada ya kuvunja mstari imara wa ulinzi wa Barlow, vikosi hivyo vikafanikiwa kuingia katika jangwa la Sinai. Katika vita hivyo vikosi vya majeshi ya Misri na Syria viliyatia hasara kubwa majeshi ya utawala wa Israel na idadi kadhaa ya ndege za kivita za Wazayuni zikasambaratishwa. Hata hivyo kutokana na hatua ya Marekani ya kuupatia silaha za kisasa utawala huo wa Kizayuni, Waarabu walipoteza baadhi ya ushindi waliokuwa wameupata katika vita hivyo.

Kikao cha makamanda wa jeshi la Kiarabu

Miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani mwaka 1981 maafisa kadhaa wa kundi la Kiislamu la "Al-Jihad" walishambulia na kumuua rais wa wakati huo wa Misri, Muhammad Anwar Sadat. Rais huyo aliuawa kwa sababu ya kutia saini makubaliano ya udhalilishaji ya Camp David mnamo mwaka 1978 na utawala ghasibu wa Israel sambamba na kuutambua rasmi utawala huo haramu. Kufuatia hatua hiyo rais huyo alihesabiwa kuwa msaliti wa malengo matukufu ya Waislamu na Waarabu. Kwa upande mwingine hatua hiyo ilipelekea kutengwa Misri baina ya nchi za Kiislamu. Ni kwa sababu hiyo ndipo makundi ya Kiislamu na wanamapambano wa Misri wakaamua kumuua Sadat, ambaye alionekana kuwa msaliti mkubwa kwa kuutambua rasmi utawala huo ghasibu unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu. Aliyetekeleza mauaji hayo alikuwa Khalid Islambuli, mmoja wa maafisa wa jeshi la Misri wakati huo. 

Picha ya mauaji ya Anwar Sadat

Na leo tarehe 6 Oktoba Misri ambayo ni moja kati ya tamaduni za kale zaidi duniani ilianzisha serikali ya jamhuri yenye bunge baada ya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Jamhuri ya Kiarabu ya Misri ina siku mbili za taifa ambazo ni tarehe 23 Julai na 6 Oktoba. Tarehe 23 Julai ni siku ya mapinduzi dhidi ya utawala wa kifalme wa Mfalme Faruq hapo mwaka 1952 mapinduzi ambayo yaliandaa uwanja wa kutangazwa jamhuri ya nchi hiyo.

Bendera ya Misri

 

Tags