Alkhamisi, Oktoba 19, 2023
Leo ni Alkhamisi tarehe 3 Mfunguo Saba Rabiuthani 1445 Hijria sawa na tarehe 19 Oktoba 2023 Milaadia.
Miaka 242 iliyopita katika siku inayofanana na ya leo, Charles Cornwallis, kamanda wa kikosi cha wanajeshi wa Uingereza nchini Marekani alisalimu amri mbele ya George Washington, kamanda wa kikosi cha wanajeshi wa Marekani na kwa msingi huo vita vya kuikomboa Marekani vikamalizika rasmi.
Vita hivyo vilianza mwaka 1775 kati ya wahajiri wa Kimarekani na wakoloni wa Kiingereza.
Miaka miwili baada ya ushindi wa mwisho wa wahajiri, pande mbili hizo zilisaini makubaliano mwaka 1783 ambapo kwa mujibu wake Uingereza ilitambua rasmi uhuru wa Marekani.
Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita yaani tarehe tarehe Tatu Mfunguo Saba Rabiuthani 1292 Hijiria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul-Qasim Kalantari Tehrani.
Alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa Kiislamu wa Tehran. Ayatullah Kalantari alibobea sana katika elimu za Hadithi, falsafa na mantiki. Msomi huyo alichota elimu kwa wasomi mashuhuri wa mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq akiwemo Shekh Murtadha Ansari na kufikia daraja ya Ijtihad.
Ameandika vitabu vingi hasa katika uwanja wa fiqhi na sheria za Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, Ali Hassan Salameh mmoja kati ya viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliuawa shahidi nchini Lebanon kupitia njama za vibaraka wa shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel, MOSSAD. S
alameh alikuwa afisa wa usalama wa PLO na aliuawa shahidi baada ya kuripuka bomu lililotegwa katika gari lake mjini Beirut.
Jinai hiyo ya utawala haramu wa Israel ndani ya Lebanon kwa mara nyingine iliweka wazi ugaidi na uvamizi wa Israel dhidi ya ardhi ya nchi nyingine.
Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita manowari za jeshi la Marekani zilishambulia visiwa vya mafuta vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Ghuba ya Uajemi wakati wa vita vya Iraq dhidi ya Iran.
Mashambulizi hayo yalifanyika baada ya Kuwait iliyokuwa ikiusaidia utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein katika vita vyake dhidi ya Iran, kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu kuwa imeshambulia meli yake ya mafuta.
Marekani ilivishambulia visiwa vya mafuta vya Iran kwa madai kuwa meli ya Kuwait iliyoshambuliwa na Iran ilikuwa na bendera ya nchi hiyo.

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, alifariki dunia Ali Ezzat Begovic, mwanasiasa na mwandishi wa Bosnia Herzegovina.
Ali Begovic alizaliwa mwaka 1925 na kupata taaluma ya sheria katika Chuo Kikuu cha Sarajevo katikati mwa Bosnia. Alianza kupambana na utawala wa kikomunisti wa Yugoslavia ya zamani akiwa kijana mdogo na kufungwa jela mara kadhaa.
Mwaka 1989 Ali Begovic aliasisi chama kipya cha siasa kwa jina la Democratic Action kilichokuwa na nafasi kubwa katika uhuru wa Bosnia mwaka 1991.
Mwanasiasa huyo wa Kiislamu ambaye baada ya uhuru wa taifa hilo alichaguliwa kuwa rais, alikuwa na nafasi kubwa katika kuwatetea raia wa Bosnia katika mashambulizi ya askari wa Serbia dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.