Oct 20, 2023 02:35 UTC
  • Ijumaa, Oktoba 20, 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 4 Mfunguo Saba Rabiuthani 1445 Hijria inayosadifiana na Oktoba 20 mwaka 2023 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1272 iliyopita, alizaliwa Sayyid Abdul Adhim al Hassani aliyekuwa mmoja wa wajukuu wa Imam Hassan al Mujtaba (a.s) huko katika mji wa Madina.

Sayyid Abdul Adhim alikuwa mmoja kati ya shakhsiya walioaminiwa na Imam al Hadi (as) na alinukuu Hadithi moja kwa moja kutoka kwa maimamu watukufu kama vile al Ridha, al Jawad na al Hadi (as).

Sayyid Abdul Adhim alihamia Iran kutokana na pendekezo la Imam al Hadi (as) kwa ajili ya kuwaongoza Waislamu na akaishi katika mji wa Rei karibu na Tehran ya sasa. Aliuawa shahidi mwezi Shawwal mwaka 250 Hijria.

Kaburi la mtukufu huyo liko katika eneo la Rei na ni miongoni mwa maeneo yanayotembelewa na Waislamu kutoka maeneo mbalimbali duniani. 

Haram ya Hadhrat Abdul Adhim

Siku kama ya leo, miaka 932 iliyopita alizaliwa mjini Baghdad Abubakr Muhammad al Anbari, faqihi, mtaalamu wa hadithi na lugha.

Anbari alipata kusoma elimu ya dini, nahwu na lugha akiwa kijana mdogo kutoka kwa baba yake. Baada ya kuhitimu masomo yake katika nyanja tofauti, alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi. Alitokea kuwa faqihi mkubwa na kutabahari katika elimu ya lugha ya Kiarabu.

Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha ‘Manshurul-Fawaaid.’ 

Siku kama ya leo miaka 196 iliyopita, inayosadifiana na 20 Oktoba 1827 kulitokea vita vya majini katika ghuba ndogo ya Navarone iliyoko kaskazini mwa bahari ya Mediteranean.

Kwenye vita hivyo, majeshi ya Uingereza, Russia na Ufaransa ambayo yalikuwa yakiiunga mkono Ugiriki, yakitumia meli za kivita, yalishambulia meli za dola ya Othmania. Nchi hizo tatu za Ulaya ziliangamiza kabisa meli 60 za kivita za dola la Othmania na kuwateka nyara wanajeshi elfu sita. 

Vita vya majini katika ghuba ya Navarone

Siku kama ya leo miaka 164 iliyopita, alizaliwa John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani.

Dewey alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na aliweza kujifunza mengi alipokuwa katika chuo kikuu cha Colombia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto.

Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni pamoja na "How we Think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture".

John Dewey alifariki dunia mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 92. 

John Dewey

Miaka 71 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, Jomo Kenyatta mwanaharakati, mwanasiasa na mpigania uhuru mashuhuri barani Afrika na Rais wa Kwanza wa Kenya alitiwa mbaroni kufuatia amri ya utawala wa kikoloni nchini Kenya.

Mzee Kenyatta alikuwa miongoni mwa watu 100 mashuhuri nchini humo waliotiwa mbaroni katika kipindi cha masaa 24 ikiwa ni katika fremu ya mpango wa kuibana Mau Mau, kundi la wapiganaji wa Kenya waliokuwa wakiupinga utawala wa kikoloni wa Waingereza.

Wakenya huadhimisha siku hii kama Sikukuu ya Mashujaa na kuwakumbuka wale wote waliopigania uhuru wa taifa hilo. ***

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi alikamatwa na wanamapinduzi karibu na mji wa bandari wa Sirte kaskazini mwa nchi hiyo na kuuawa.

Gaddafi aliuawa baada ya miezi kadhaa ya mapigano na wanamapinduzi ambapo jeshi lake liliwaua maelfu ya wananchi hususan katika miji ya Benghazi na Tripoli.

Gaddafi ambaye aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 42 alizaliwa mwaka 1942. Aliingia madarakani mwaka 1969 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani mfalme Mohammad Idris al-Sanusi. 

Kanali Muammar Gaddafi