Oct 22, 2023 02:34 UTC
  • Jumapili, Oktoba 22, 2023

Leo ni Jumapili 6 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1445 Hijria ambayo inasadifiana na 22 Oktoba 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1320 iliyopita, alifariki dunia Hisham Bin Abdul-Malik, kiongozi wa 10 katika silsila ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuwa madarakani kwa karibu kipindi cha miaka 20. Hisham aliyekuwa mtawala dikteta, alizaliwa mwaka 72 Hijria na kushika uongozi wa Waislamu mwaka 105 Hijria. Hisham alikuwa mashuhuri kwa kuwa bahili, katili na dhalimu, ambaye aliwakandamiza Waislamu wa zama zake hususan wafuasi wa Ahlulbait wa Mtume (saw). Mtawala huyo wa Bani Umayyah aliishi katika kipindi cha Imam Muhammad Baqir (as) mmoja wa wajukuu watukufu wa Nabii wa Muhammad (saw) na alimfanyia maudhi mengi mtukufu huyo na baadaye kutoa amri ya kuuawa kwake. Mbali na hapo Hisham alifanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya harakati ya Zaid bin Ali, mjukuu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as). Baada ya kuuliwa Zaid, mtawala huyo dhalimu alitoa amri ya kuchomwa moto mwili wa mtukufu huyo. Licha kwamba katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah, Uislamu ulienea maeneo ya mashariki na magharibi mwa dunia, lakini kulishuhudiwa harakati kadhaa za Kiislamu za kupinga dhulma, kutokana na kushadidi dhulma na ukandamizaji wa Hisham bin Abdul-Malik, harakati ambazo zilipelekea kudhoofika kwa dola hilo la Bani Umayyah. ***

 

Siku kama ya leo miaka 629 iliyopita alifariki dunia Mir Sayyid Sharif Gorgani, mtaalamu wa fasihi wa Iran huko Shiraz. Gorgani alizaliwa mwaka 740 Hijiria karibu na mji wa Gorgani ya leo, kaskazini mwa nchi hii. Mir Sayyid Sharif Gorgani alihesabika kuwa msomi mkubwa katika zama hizo hususan katika uga wa elimu ya fasihi. Ameacha athari mbalimbali mojawapo ikiwa ni kitabu kiitwacho "Risaalatul-Kubra fil-Mantwiq" na "Sharhu Mawaaqif Qadhi Adhdud-Diin Iji." ***

Kaburi la Mir Sayyid Sharif Gorgani

 

Siku kama ya leo miaka 593 iliyopita, sawa na tarehe sita Rabiuthani mwaka 852 Hijiria, alizaliwa Ebn Eyas, mwanahistoria mashuhuri wa Misri. Ebn Eyas alinakili habari mbalimbali za kihistoria kwa mfumo wa nathari nyepesi, mfumo ambao ulikuwa hautumiwi na wanahistoria wengine. Mfumo huo ulikuwa na umuhimu mkubwa kwenye taaluma ya lugha ya Kiarabu. Miongoni mwa athari muhimu ya kihistoria za Ebn Eyas ni pamoja na kitabu cha "Badaaiuz-Zuhuur fii Waqaaiud-Duhuur" ambacho kinaelezea historia ya Misri tangu karne za nyuma hadi kipindi chake. Aidha alifafanua maisha ya watawala wa Misri, ujenzi na uimarishwaji wake na mambo mbalimbali yaliyowahi kuikumba nchi hiyo katika karne za nyuma. ***

Ebn Eyas

 

Miaka 117 iliyopita katika siku kama ya leo, Paul Cezanne mchoraji maarufu wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67. Alikuwa na shauku na mapenzi makubwa na fani ya uchoraji tangu akiwa mdogo, lakini kutokana na msisitizo wa baba yake aliingia Chuo Kikuu na kusoma taaluma ya sharia. Hatimaye akiwa na umri wa miaka 24, baba yake alimruhusu kuendelea na masomo katika taaluma ya uchoraji. Mwanzoni mabango ya uchoraji ya Paul Cezanne hayakupata wafuasi wengi na athari zake za uchoraji zilikabiliwa na ukosoaji mkubwa. Mwenendo huo uliendelea hadi alipofikisha umri wa miaka 50 ambapo hatua kwa hatua alianza kupata umashuhuri kutokana na kuuza mabango yake ya uchoraji. ***

Paul Cezanne

 

Tarehe 30 Mehr miaka 71 iliyopita, Dakta Hussein Fatimi, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Dakta Musadiq, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Iran wakati huo alitangaza habari ya kukatwa uhusiano wa kisiasa kati ya Iran na Uingereza. Uamuzi huo ulikabidhiwa kwa balozi mdogo wa Uingereza mjini Tehran, baada ya kuidhinishwa na baraza la mawaziri. Dakta Fatimi alisema Tehran imeamua kukata uhusiano na Uingereza kutokana na upuuzaji wa serikali ya London kwa matakwa ya wananchi wa Iran ya kujipatia haki zao, hususan katika uwanja wa kutaifisha sekta ya mafuta. Dakta Fatimi aliwataka viongozi wa London wabadili siasa zao kuhusiana na Iran. ***

Dakta Hussein Fatimi

 

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, aliaga dunia Arnold Joseph Toynbee mwanahistoria mtajika wa Uingereza. Alizaliwa mwaka 1889. Toynbee alikuwa akifundisha taaluma ya Historia ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha London. Msomi huyo ameandika vitabu vingi katika uga wa historia na baadhi ya vitabu vyake ni A Study of History, Change and Habit, Choose Life na Civilization on Trial. ***

Arnold Joseph Toynbee

 

Miaka 12 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud aliyekuwa mrithi wa kiti cha Ufalme wa Saudia. Sultani alikuwa mtoto wa 15 wa kiume wa Mfalme Abdul-Aziz na mama yake ni Hussa Bint Ahmed Al-Sudairi. Vyombo vya Saudi vilitangaza kuwa, mwanamfalme Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud aliaga duniia katika moja ya hospitali mjini New York Marekani. Sultan bin Abdul-Aziz aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 85 baada ya maradhi ya saratani kuenea katika mwili wake wote. ***

Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud

 

Na tarehe 22 Oktoba ni siku ya kitaifa ya Vatican, inayohesabiwa kuwa nchi ndogo zaidi duniani. Vatican ina ukubwa wa chini ya nusu kilomita mraba, na jamii ya watu karibu elfu moja huko kusini mwa bara Ulaya. Nchi hiyo iko eneo la magharibi ndani ya mji mkuu wa Italia, Roma. Lugha rasmi ya Vatican ni Kitaliano. Wakazi wa Vatican ni wafuasi wa madhehebu ya Katoliki na wanatumia sarafu ya Yuro. Nchi hiyo ndogo ya Vatican inatawaliwa na serikali ya kidini ambayo inaongozwa na Papa wa Kanisa Katoliki. Vatican inatajwa kuwa kituo kikuu cha kupanga mikakati ya madhehebu ya Katoliki katika maeneo mbalimbali duniani. Nchi ya Vatican ilijitenga na Italia mwaka 1929 na tarehe 22 Oktoba ya kila mwaka ambayo kwa hakika ni siku ya kuchaguliwa Papa John Paul wa Pili hapo mwaka 1978, imetangazwa kuwa ni Siku ya Kitaifa ya Vatican. ***

Bendera ya Vatican