Jumatatu, tarehe 23 Oktoba, 2023
Leo ni Jumatatu tarehe 7 Mfunguo Saba Rabiuthani 1445 Hijria mwafaka na tarehe 23 Oktoba 2023.
Katika siku kama ya leo miaka 213 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Abul-Feidh Hamdun Ibn Abdul-Rahman mashuhuri kwa jina la Ibn Haj, mfasiri, mwanafasihi na fakihi wa Kiislamu aliaga dunia.
Alizaliwa mwaka 1174 Hijria katika moja ya miji ya leo ya Morocco na kukulia huko.
Ibn Abdul-Rahman alisoma elimu za fasihi na dini kwa walimu na maustadhi mashuhuri wa zama hizo. Alimu na mwanazuoni huyu alikuwa mahiri pia katika uandishi wa vitabu ambapo ana vitabu mbalimbali katika elimu za fikihi, teolojia, tafsiri, mantiki na elimu nyigine.

Miaka 151 iliyopita, aliaga dunia Theophile Gautier, malenga na mwandishi wa Kifaransa. Gautier alizaliwa mwaka 1811 na kuhitimu masomo yake huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa.
Theophile Gautier kwa muda fulani alikuwa mwandishi wa gazeti na alikuwa na hamu kubwa ya kuwa mchoraji au mwanamuziki. Lakini hatimaye alijifunza fasihi hususan mashairi na kuacha athari maarufu katika uwanja huo.
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, vita vya kihistoria vilivyopewa jina la al-Alamein vilitokea katika mji wenye jina kama hilo huko kaskazini mwa Misri kati ya wanajeshi wa Uingereza na jeshi la Manazi wa Ujerumani.
Vita hivyo vilimalizika baada ya kushindwa jeshi la Ujerumani, japokuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika.
Amani kamili ilipatikana katika maeneo hayo baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Na miaka 46 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Sayyid Mustafa Khomeini, mtoto wa Imam Ruhullah Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa shahidi kufuatia njama ilizofanywa na askari usalama wa utawala wa Shah akiwa nyumbani kwake huko Najaf, moja kati ya miji mitukufu ya Iraq.
Al Haj Mustafa Khomeini alizaliwa mwaka 1309 Hijria Shamsiya katika mji mtakatifu wa Qum na baadaye akajiunga na chuo cha elimu ya dini cha mji huo kwa ajili ya masomo ya juu baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Alikuwa hodari mno na alifikia daraja ya juu ya kielimu ya Ijtihadi akiwa na umri wa miaka 27.
Ayatullah Mustafa Khomeini alikuwa pamoja na baba yake Imam Khomeini katika kipindi chote cha mapambano dhidi ya utawala wa Shah.