Alkhamisi, Oktoba 26, 2023
Leo ni Alkhamisi tarehe 10 Mfunguo Saba Rabiuthani 1445 Hijria sawa na Oktoba 26 mwaka 2023 Milaadia.
Miaka 1244 iliyopita inayosadifiana na tarehe 10 Rabiuthani mwaka 201 Hijria, alifariki dunia Bibi Fatima Maasuma A.S, binti wa Imam Mussa bin Jaafar al-Kadhim (as).
Bibi Fatima Maasuma alizaliwa mwaka 173 Hijria katika mji wa Madina. Alikuwa mwanamke mwenye fasaha katika uzungumzaji, alimu, hodari na zahidi na mcha- Mungu.
Mwaka mmoja baada ya kaka yake yaani Imam Ali bin Mussa Ridha (as) kuwasili Khurasan nchini Iran, Bibi Maasuma aliondoka Madina kwa lengo la kumfuata kaka yake, lakini akiwa njiani alisimama katika mji wa Qum na kufariki dunia mjini humo kutokana na maradhi au kwa mujibu wa kauli nyingine, kutokana na sumu aliyeopewa.

Tarehe 10 Rabiuthani mwaka 1330 Hijria yaani siku kama hii ya leo miaka 115 iliyopita Haramu tukufu ya Imam Ali bin Mussa Ridhaa, mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Mash'had huko kaskazini mwa Iran ilishambuliwa kwa mizinga na wavamizi wa Kirusi.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Mmarekani, Morgan Shuster kuanzisha kikosi maalumu cha polisi ya Hazina Kuu ya Iran.
Urusi iliitambua hatua hiyo kuwa ni kinyume na maslahi yake haramu nchini. Mashambulizi hayo yalisababisha hasara kubwa kwa haramu ya mjukuu huyo wa Mtume (saw) na mali za thamani za eneo hilo tukufu ziliporwa na wavamizi hao.
Miaka 76 iliyopita katika siku kama hii ya leo eneo la kiistratejia la Jammu na Kashimir liliunganishwa na India baada ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza na Pakistan kujitenga na India.
Ilipangwa kuwa, eneo la Jammu na Kashmir lenye wakazi wengi Waislamu litajiunga na Pakistan lakini mtawala wa eneo hilo akichochewa na India na Uingereza, aliamua kuliunganisha na India na kupuuza matakwa ya wananchi. Baada ya kutangazwa habari hiyo Pakistan ililishambulia eneo hilo na kutwaa sehemu ya Jammu na Kashmir.
Tangu wakati huo hadi sasa India na Pakistan zimepigana vita mara mbili juu ya umiliki wa eneo la Jammu na Kashmir na hitilafu za pande hizo mbili zingali zinaendelea.

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, Imam Ruhullah Khomeini baada ya kuachiwa huru kutoka katika jela ya utawala wa Shah alitoa hotuba kali akishambulia vikali kitendo cha kupasishwa sheria ya Capitulation au sheria ya kuwapatia kinga ya kutofikishwa mahakamani raia wa Marekani waliofanya uhalifu nchini Iran.
Katika hotuba hiyo Imam Khomeini alizishambulia vikali Marekani na utawala ghasibu wa Israel.
Hotuba hiyo iliwaamsha wananchi na kuukasirisha utawala wa kiimla wa Shah kiasi kwamba uliamua kumuwekea vizuizi vingi kiongozi huyo wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu. Siku chache baadaye Imam alipelekwa uhamishoni nchini Uturuki na baadaye Iraq.

Katika siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, televisheni ya taifa ya Iran ilianza kurusha matangazo yake kwa majaribio.
Katika muongo wa 1330 Hijria Shamsia kulijadiliwa suala la kuanzishwa televisheni ya taifa ya Iran ingawa utekelezaji wa mpango huo uliakhirishwa kwa miaka mingi. Uzalishaji wa picha tena kwa masaa kadhaa tu, halikuwa jambo rahisi kwani lilihitajia fedha na uwekezaji binafsi na wa kila wiki.
Ni kwa msingi huo, ndio maana Habibullah Thabit Pasal mwekezaji wa sekta binafsi akaipendekezea serikali ya wakati huo ya Iran ianzishe mnara wa televisheni, pendekezo ambalo lilikubaliwa.
Baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran redio na televisheni ya taifa ilibadilishwa jina na kuwa Shirika la Utangazaji la Radio na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kupiga hatua kubwa mno katika uwanja huo.
Hii leo shirika hili lina makumi ya kanali za televisheni na radio zikiwemo zile za kitengo cha matangazo ya ng'ambo ambapo kuna makumi radio na televisheni za lugha za kigeni kama, Kiingereza, Kifaransa, Kiswahili, Kihispania, Kiarabu, Kihindi, Kipashto, Kijapan, Kiurdu, Kihausa na kadhalika.

Miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo, mji wa Khorramshahr wa Iran ulikaliwa kwa mabavu na jeshi la dikteta wa zamani Iraq Saddam Hussein.
Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu mwaka mmoja na miezi minane.
Mji huo ulikombolewa tarehe 3 Khordad ambayo inajulikana katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa jina la "Siku ya Istiqama na Ushindi.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita maajenti wa shirika la ujasusi la Israel Mossad walifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya Katibu Mkuu wa zamani wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, Dakta Fat'hi Shiqaqi, akiwa huko Malta.
Shiqaqi alizaliwa mwaka 1951 katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza.
Alihitimu masomo ya udaktari na kufanya kazi katika hospitali moja ya Baitul Muqaddas. Alianzisha harakati za mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel akiwa bado kijana.
Mwaka 1979 Dakta Shiqaqi alikamatwa na kusweka jela nchini Misri kwa sababu ya kuandika kitabu kuhusu harakati za Imam Ruhullah Khomeini na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Dakta Shiqaqi aliitangaza Siku ya Kimataifa ya Quds iliyoainishwa na Imam Khomeini, kuwa ni siku ya kuhuisha Uislamu na mapambano ya jihadi dhidi ya Wazayuni huko Palestina.